Mfanyabiashara Kizimbani kwa Mashitaka 28 ya Uhujumu Uchumi

Mkurugenzi wa kampuni ya Jaluma General Supplies Limited,  Lucas Mallya  na wenzake wanane wamefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu wakikabiliwa na mashtaka 28 yakiwemo ya  kukwepa kodi na kuisababishia Serikali  hasara ya zaidi ya Sh31.57 bilioni.

Mbali na Mallya washtakiwa wengine ni Emmanuel Peter,  mkurugenzi wa Happy Imports Assosiates, Happy Mwamugunda; Prochesi Shayo; Prokolini  Shayo;  Godfrey Urio;  Nyasulu Nkyapi; Tunsubilege Mateni na Nelson Kahangwa

Akisoma mashtaka hayo jana Jumatano Januari 29, 2020 mbele ya Hakimu mfawidhi, Godfrey Isaya wakili wa Serikali, Faraja Ngukah alidai washtakiwa walitenda makosa hayo kati ya Januari Mosi, 2015 na Januari 7, 2020 maeneo mbalimbali ya Jiji la Dar es Salaam.

Washitakiwa hao hawakutakiwa kujibu chochote kwa sababu mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikiliza kesi za uhujumu uchumi.

Hata hivyo, upande wa mashtaka ulidai upelelezi wa kesi hiyo unaendelea hivyo, waliomba tarehe nyingine kwa ajili ya kutajwa na kukamilisha upelelezi.

Hakimu Isaya aliahirisha kesi hiyo hadi Fabruari 12, 2020 kwa ajili ya kutajwa na washtakiwa walipelekwa rumande kwa sababu mashtaka ya utakatishaji fedha hayana dhamana kisheria.


from MPEKUZI

Comments