CHADEMA Yawataka wanaotaka Kugombea Nafasi Mbalimbali 2020 Waandike Barua za Kuonesha Nia

Chama  cha Chadema kimewataka wanachama wa chama hicho wenye nia ya kugombea nafasi mbalimbali kwenye uchaguzi mkuu wa Oktoba 2020 waandike barua za kuonyesha nia.

Hayo yamesemwa leo Jumatano Januari 29, 2020 na Katibu Mkuu wa Chadema, John Mnyika wakati wa mahojiano maalum yaliyorusha Kituo cha Televisheni cha ITV.

Mnyika amesema hayo baada ya kuulizwa na mtandazaji kwenye mahojiano hayo kama Chadema wanatarajia kumsimamisha aliyekuwa mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu kugombea nafasi ya urais kwa tiketi ya chama hicho kwenye uchaguzi mkuu ujao.

“Waswahili wanasema linalosemwa lipo, ni kweli kwamba mnataka kumsimamisha Lissu kugombea nafasi ya urais mwaka 22020?” alihoji mtangazaji wa kipindi hicho, Farhia Middle

Akijibu swali hilo, Mnyika amesema, “mimi ni msimamizi wa uchaguzi na uteuzi wa mgombea ni sehemu ya uchaguzi, naomba kwa sasa nisiseme chama kinalenga kumsimamisha nani kugombea urais na katiba ya chama chetu inasema kamati kuu ndiyo yenye mamlaka ya kutafiti jina la mgombea urais.”

“Ila watanzania wawe na uhakika, Chadema itasimamisha mgombea wa urais ambaye ana uwezo wa kushinda na kuleta mabadiliko ya kweli.”

Amesema kwa sasa chama kinawaalika wanachama na wasio wanachama wenye nia ya kugombea nafasi mbalimbali katika uchaguzi mkuu ujao waandike barua kuonyesha nia zao.


from MPEKUZI

Comments