WanaCCM watakiwa kutoa maoni kuhusu Ilani ya mwaka 2020-2025

Halmashauri kuu ya Taifa imeagiza wana chama wa Chama cha Mapinduzi (CCM) kupitia kamati za mikoa na wilaya nchini kutoa maoni kuhusu ilani ya mwaka 2020/2025.

Kauli hiyo imetolewa na Katibu mkuu wa CCM Taifa, Dkt Bashiru Ali wakati akizungumza na wananchi na viongozi mbalimbali wa chama hicho katika eneo la Bujunangoma katika Halmashauri ya wilaya ya Bukoba mkoani Kagera alipopata nafasi ya kukagua Mradi wa ujenzi wa hospitali ya wilaya hiyo.

Dkt Bashiru amesema ni mhumu maoni hayo yatolewe ambapo kila wilaya itatakiwa kuyapeleka mkoani na mkoani kuyafikisha taifani na kuwa zoezi hilo litafungwa Januari 15, 2020.

Katibu huyo amesema jambo hilo ni muhimu sana hasa pale muda husika ukizingatiwa kwani baada ya zoezi hilo la ukusanyaji kuisha maoni hayo yatachakatwa na kamati husika inayoandaa ilani ili kuwa na ilani bora zaidi kuliko inayomalizika.

Amewapongeza watanzania kwa mafanikio yaliyopatikana katika kipindi hiki cha Rais wa Jamhuli ya Muungano wa Tanzania Dkt John Pombe Joseph Magufuli kwani mafanikio hayo yametokana na kodi za wananchi na pia nidhamu yawatumishi ndani ya serikali.

Aidha amewataka watanzania kuendelea kushikamana, kulinda amani kama Rais Magufuli anavyohimiza kubwa zaidi akiomba kukiamini chama cha mapinduzi.

"Imani tunayopewa na wananchi ifanane na namna tunavyoendesha siasa ndani ya chama chetu" alisema Katibu mkuu huyo.

Aidha amewapongeza wananchi Mkoa Kagera kwa ushindi mkubwa walioupata kwa 100% katika Halmashauri ya wilaya Bukoba katika uchaguzi wa serikali za mitaa ulioisha.

Hata hivyo amesema chama hicho kimejipanga vizuri katika kuelekea uchaguzi mkuu ujao wa 2020 na kuongeza kuwa wataahidi watakayoyafanya zaidi.


from MPEKUZI

Comments