Waziri Mhagama Ampa Miezi Miwili Mkandarasi Kukamilisha Hatua Ya Kwanza Kiwanda Cha Bidhaa Za Ngozi Cha Karanga.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Kazi, Ajira, Vijana na Watu wenye Ulemavu) Mhe. Jenista Mgahama, amempa miezi miwili mkandarasi anayejenga Kiwanda cha bidhaa za ngozi cha Karanga, kilichopo mkoani Kilimanjaro, kukamilisha hatua ya kwanza ya  ujenzi wa kiwanda hicho hadi kufikia tarehe 20 Januari mwaka 2020, ili ujenzi  hatua ya pili ya ujenzi wa kiwanda hicho uweze kuanza mara moja kwa ajili ya kuhakikisha kiwanda kinaanza uzalishaji wa bidhaa za ngozi.

Mkandarasi huyo ambaye ni Kikosi cha ujenzi cha Shirika la Uzalishaji la Magereza ameelekezwa kufanya kazi usiku na mchana ili kuhakikisha ndani ya kipindi hicho kuhakikisha amejenga majengo manne, ikiwa ni jengo la kuzalisha bidhaa za ngozi na soli za viatu, jengo la mitambo ya umeme pamoja na ghala la vifaa vya ngozi.

Waziri Mhagama ametoa maelekezo hayo mara baada ya kukagua maendeleo ya ujenzi wa kiwanda hicho leo tarehe 29 Novemba, 2019, mkoani Kilimanjaro, ambapo amefafanua kuwa  kiwanda hicho ni muhimu kujengwa kwa haraka sana kwani kitaiwezesha Tanzania  kuufikia uchumi wa viwanda kwa kuwa bidhaa zitakazozalishwa na kiwanda hicho zina soko kubwa ndani na nje ya nchi hususani katika Jumuiya ya maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC).
 
“Sisi katika Afrika ni matajiri wa mifugo na bidhaa zinazolishwa na mifugo, lakini hapa nchini  hatuna kiwanda tunachoweza kutegemea katika bidhaa za ngozi, hivyo ni muhimu kuharakisha ujenzi wa kiwanda hiki ili tuweze kutengeneza ajira hapa kati ya elfu tatu hadi elfu nne na ukizingatia nguvu kazi ya nchi yetu asilimia 56 ni vijana.Kiwanda hiki kitakuwa muhimu sana kwa ustawi wa nchi” Amesema Mhagama.

Mhe. Mhagama amewataka watekelezaji wa Mradi huo  kuhakikisha wanakuwa na mpango kazi wa kukamilisha kazi hiyo na kuuwasilisha kwake, lakini pia kuwa  na mpango mkakati wa biashara utakao wezesha kusaidia kupatikana na masoko ya bidhaa hizo. Ameongeza kuwa atakuwa na watu wakufuatilia kwa karibu shughuli za ujenzi huo ili kuhakikisha ujenzi unakamilika kwa wakati. Huku akisisitiza Changamoto zozote za utekelezaji wa Mradi huo zizingatiwe ili pindi ukikamilika zisije anza kuibuliwa na kuweza kukukosesha mradi kufikia malengo yaliyokusudiwa.

Kwa upande wake Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi,Ajira, vijana na Watu wenye Ulemavu), Andrew Massawe, amemuhakikishia Mhe. Waziri Mhagma kuwa, atafuatilia ushughuli za ujenzi wa mradi huo kwa  karibu ili kuhakikisha maelekezo yake yanatekelezwa kwa  kila hatua za ujenzi ili kuhakikisha ujenzi unakamilika kwa muda uliopangwa.

Naye, Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma, Hosea Kashimba amemhakikishia Mhe.Waziri Mhagama kuwa atahakiksha kuwa ujenzi huo unakuwa na ubora na unakamilika ndani ya muda aliouelekeza ili watanzania waweze kunufaika na  bidhaa za kiwanda hicho lakini pia waweze  kupata ajira za uhakika kutoka katika kiwanda hicho.

Utekelezaji wa Mradi wa Ujenzi wa Viwanda vya ngozi Karanga unatekelezwa na Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF),na Magereza kupitia wataalamu wake wa ndani na timu ya washauri elekezi wa viwanda TRIDO.

Mradi wa ujenzi wa Kiwanda cha bidhaa za ngozi cha Karanga unatokana na Kampuni ijulikanayo kwa jina la “Karanga leather Industries Co Ltd” iliyoanzishwa mwaka 2017  kwa lengo la kutekeleza mradi wa viwanda vya bidhaa za ngozi katika eneo la gereza la Karanga , kampuni hiyo iliingia ubia kati  ya uliokuwa mfuko wa Pensheni PPF ambapo kwa sasa majukumu yake yamechukuliwa na PSSSF pamoja na Jeshi la Magereza kupitia Shirika la Uzalishaji. Malengo ya ubia huo nikuongeza wigowa uzalishaji wa bidhaa za ngozi na kuongeza thamani ya ngozi nchini.

MWISHO.


from MPEKUZI

Comments