Rais Magufuli amempongeza Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga (RC), Zainabu Tellack kwa kumwakilisha vema kwa kusimamia kikamilifu nafasi yake na kupambana na rushwa.
Akizungumza na wananchi eneo la Isaka Wilaya ya Kahama mkoani Shinyanga leo Jumatano Novemba 27, 2019, Rais Magufuli amemtaka mkuu huyo wa mkoa kuchapa kazi na kuendelea kupiga vita vitendo vya rushwa kwenye eneo lake.
“Mkuu wa mkoa wewe unafanya kazi nzuri sana; endelea kufanya kazi. Wewe ndiye mwakilishi wangu hapa na mwenyekiti wa kamati ya ulinzi na usalama ya Mkoa...ndio maana nimewasimamisha kazi RPC na RCO. Sijui walikuwa wanakudharau kwa sababu wewe ni mwanamke?” amesema Rais Magufuli
Rais Magufuli ametoa kauli hiyo siku chache baada ya kuagiza kusimamishwa kazi kwa Kamanda wa Polisi mkoa (RPC) wa Shinyanga, Richard Abwao, Mkuu wa Upelele wa mkoa (RCO), John Rwamlema na Meneja wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) wa mkoa huo, Jumbe Samson kwa tuhuma za utovu wa nidhamu na uhujumu uchumi.
Kusimamishwa kazi kwa vigogo hao wa mkoa kulitokana na madai ya kushindwa kutekeleza maelekezo ya mkuu wa mkoa kuhusu hatua za kisheria dhidi ya kampuni moja inayozalisha pombe kali inayodaiwa kukwepa kodi.
from MPEKUZI
Comments
Post a Comment