Watu wasiopungua 70 wameuwawa na dazeni kadhaa kujeruhiwa baada ya jiko la gesi kuripuka ndani ya treni iliyokuwa ikiwasafirisha waumini waliokuwa njiani kwenda kufanya ziara ya kidini nchini Pakistan.
Picha za televisheni zinaonyesha moto unaofuka ndani ya mabehewa matatu ya treni huku vilio vikisikia ndani ya treni hiyo katika eneo la vijijini la mkoa wa kati wa Punjab.
Baadhi ya abiria-wengi wao wakiwa waumini waliokuwa njiani kwenda katika ziara ya kidini katika mji wa mashariki wa Lahore, walikuwa wakipika chakula cha asubuhi pale majiko yao mawili ya gesi yaliporipuka-Ali Nawaz, afisa wa ngazi ya juu wa shirika la safari za reli la Pakistan ameliambia shirika la habari la Ufaransa AFP.
Wapakistan wengi wanabeba vyakula wanapokuwa katika safari ndefu lakini majiko ya gesi yamepigwa marufuku. Ali Nawaz anasema uchunguzi unafanywa kuhusu ajali hiyo.
Televisaheni za Pakistan zimeonyesha jinsi dazeni za watu walivyokusanyika njiani kuangalia jinsi moto unavyofuka ndani ya mabehewa ambayo yaliachana na sehemu nyengine ya treni.
Waziri Mkuu Imran Khan ameamuru uchunguzi juu yakisa hicho kufanywa mara moja
Vikosi vya zimamoto vimefika haraka katika eneo hilo karibu na wilaya ya Rahim Yar Khan. Watumishi wa mashirika ya uokozi na wanajeshi pia wameonekana wakisaidia. Miili ya wahanga wa ajali hiyo iliyofunikwa shuka nyeupe imekuwa ikiondolewa.
from MPEKUZI
Comments
Post a Comment