Mvua yasababisha mafuriko wilayani Korogwe.....Mamia ya abiria wakwama

Mamia ya abiria waliokuwa wanasafiri kutoka Arusha, Kilimanjaro na nchi jirani na waliotoka Dar es Salaam kuelekea mikoa mbalimbali wamekwama tangu jana mchana Ijumaa Oktoba 25, 2019 wilayani Korogwe na Handeni Mkoa wa Tanga.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tanga, Edward Bukombe, amesema kuwa Jeshi la Polisi mkoani humo linaendelea kuimarisha usalama kwa abiria wote, waliokwama kuendelea na safari baada ya maji kujaa juu ya daraja ili kuepusha madhara makubwa hususani wale ambao watalazimisha kuvuka.

Kauli hiyo ameitoa leo ambapo amesema kuwa abiria ni wengi kwani wanaongezeka kila muda na kwamba wameshindwa kupata idadi kamili ya watu waliokwama kwa hizo pande zote mbili.

"Bado njia haijafunguka kule Handeni tulikokuwa tunapategemea kupita daraja lilishakatika kabisa kwahiyo hakuna mawasiliano na hii ya Segera - Korogwe na yenyewe bado maji yanapita juu, kwahiyo tunasubiri maji yapungue ili tuone uimara wa daraja na gari kama zinaweza zikapita", amesema Kamanda Bukombe.

"Tunachokifanya kwa sasa ni kuimarisha ulinzi ili yasiwepo madhara ya kuibiwa na wale ambao huwa wanataka kuvuka kwa kutumia nguvu'', ameongeza.

Inakadiriwa kuwa abiria zaidi ya 5,000, kutoka mikoa ya Arusha, Kilimanjaro na hata nchi jirani na wale waliokuwa wanatoka Dar es Salaam kwenda katika mikoa hiyo wamekwama siku ya jana ya Oktoba 25, 2019, wilayani Korogwe na Handeni, kufuatia mvua kubwa inayonyesha na kupelekea maji kujaa juu ya daraja na huku lingine likisombwa na maji.
 


from MPEKUZI

Comments