Wakati Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Rais John Pombe Magufuli inaendelea kujenga miradi mikubwa ya kimkakati ya kuelekea katika uchumi wa kati bado Mkoa wa Kagera haujasaulika bali sasa wananchi wake wanakumbushwa kujiandaa kikamilifu kwa kuchapa kazi za kilimo na biashara wakati nchi inaelekea katika mapinduzi makubwa ya kiuchumi ili kutembea na kasi ya uchumi wa kati.
Ni baada ya meli ya MV Victoria meli kongwe na maarufu kwa wakazi wa Mkoa wa Kagera kukamilika ukarabati wake ifikapo Machi 2020 na kurejea katika Ziwa Victoria kwa kufanya kazi kati ya bandari za Mwanza, Bukoba na Kemondo kusafirisha abiria zaidi 1000 pamoja na mizigotani 200 ambapo kutakuwepo na nafuu kubwa ya bidhaa za viwandani pamoja na usafiri wa wananchi kati ya Bukoba na mwanza.
Uhakika wa meli ya MV Victoria kukamilika ukarabati wake mwakani Machi 2020 pia na ujenzi wa meli mpya ulishuhudiwa na Mkuu wa Mkoa wa Kagera Brigedia Jenerali Marco E. Gaguti pamoja na Kamati ya amani ya Mkoa wa Kagera iliyowajumuisha viongozi wa dini watatu Askofu Methodius Kilaini Askofu msaidizi Jimbo Katoliki la Bukoba, Askofu Dk. Abednego Keshomshahara Askofu wa (KKKT) Jimbo la Kasikazini Magharibi na Sheikh Haruna Kichwabuta Sheikh wa Mkoa wa Kagera.
Mkuu wa Mkoa Gaguti akiwa katika ziara hiyo ya kutembelea na kujionea maendeleo ya ukarabati na ujenzi wa Meli mpya pamoja na cherezo katika Bandari ya Mwanza Kusini alisema kuwa anampongeza Rais Magufuli kwa kuleta mradi huo kwa ajili ya ukombozi wa kiuchumi wa wananchi wa Kagera kwani utaweka usafiri wa uhakika pia alitoa wito kwa wananchi wa Kagera kujielekeza katika kazi zenye tija za kilimo na biashara na kujiandaa kutumia maboresho ya usafiri kuinua uchumi wa mkoa.
Askofu Msaidizi Methodius Kilaini baada ya kuiona miradi hiyo mitatu alisema kuwa anamshukuru Rais John Pombe Magufuli kwa kutekeleza maajabu katika miradi ya ujenzi na ukarabati wa meli, aidha alisema kuwa Mkuu wa Mkoa Gaguti amewafanyia jambo jema sana la kuwafanya wao kama viongozi wa dini wapate nguvu ya kuleta tumaini na uelekeo kwa watu na kuufanya Mkoa wa Kagera kusimama tena kiuchumi.
Askofu Dk. Keshomshahara mara baada ya kujionea ujenzi wa meli mpya na cherezo na ukarabati wa Meli ya MV Victoria alisema kuwa sasa wao kama viongozi wa dini wamepata neno la kuwaeleza waamini wao na kuwahamasisha kujiandaa kwaajili ya kuitumia fursa ya Meli hizo zikikamilika . Sheikh Haruna Kichwabuta naye alisema kuwa Rais Magufuli alihaidi wakati wa kampeini sasa ametekeleza bila ahadi hewa hasa kwa wananachi wa Mkoa wa Kagera.
Bw. Eric B. Hamissi Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya Huduma za meli nchini alimshukuru Mkuu wa Mkoa wa Kagera Mhe. Gaguti kutembelea miradi hiyo ya ujenzi na ukarabati wa meli na kutoa wito kwa wananchi na viongozi wengine nchini kwenda kutembelea miradi hiyokujionea maendeleo ya ujenzi wa meli mpya na cherezo pia na ukarabati wa meli za zamani.
Bw. Eric alisema kuwa mradi unatekelezwa na Kampuni ya JV of Gas Entec CO. Ltd Kang Nam Corporation na SUMA JKT ambapo kwa ujumla utagharimu jumla ya shilingi bilioni 152 na tayari Serikali imetoa shilingi bilioni 60 wakandarasi wanadaiwa kazi hawaidai Serikali aidha, mradi umegawanyika katika sehemu kuu nne. Kwanza ni ujenzi wa meli mpya ambayo itakuwa na uwezo wa kubeba tani 400 Abiria 1200 ikiwa na urefu wa meta 92.6, urefu kwenda juu meta 11.2 (sawa na ghorofa nne) na upana wa meta 17 na gharama yake ni shilingi bilioni 90.
Mradi wa pili ni ujenzi wa cherezo ambacho kitakuwa na uwezo wa kubeba meli zenye uzito wa tani 4000 ambapo meli mpya itakuwa na uzito wa tani 3500 tu aidha, cherezo kama hicho hakuna katika nchi za Afrika Mashariki na Kati na kikikamilika kitaiingizia Serikali Mapato kama kitatumika kwa kujenga meli zenye uzito mkubwa hasa kutoka nje ya Tanzania. Mradi wa cherezo utagharimu shilingi bilioni 36 na ujenzi wake umefikia asilimia 52.
Mradi wa tatu ni ukarabati wa Meli ya MV Victoria ambao utagharimu shilingi bilioni 22.8 na ukarabati wa meli hiyo umefikia asilimia 50 ambapo inakarabatiwa ikiwa ni pamoja na kubadilishwa mfumo wake wa zamani na kuwekewa mfumo wa kidigitali. Mradi wa wa nne ni ukarabati wa meli ya Butihama ambapo mradi huo nao utagharimu shilingi bilioni 4.9 na ukarabati wake umefikia asilimia 40.
Kwa msaada wa ofisi ya mkuu wa mkoa
from MPEKUZI
Comments
Post a Comment