Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu amesema kuwa maambukizi ya VVU yamepungua kutoka asilimia 7 mwaka 2003/4 hadi asilimia 4.7 mwaka 2016/17.
Waziri Ummy amesema hayo jana wakati wa mkutano wa kujadili maendeleo ya utekelezaji wa sera ya pamoja ya ushirikiano na Serikali ya Marekani kupitia PEPFAR cop 19 kuhusiana na masuala ya VVU na UKIMWI uliofanyika jijini Dar Es Salaam. “Kuanzia huduma za UKIMWI zianze kutolewa nchini tumeshuhudia mafanikio makubwa kwa upande wa kupunguza maambukizi kutoka asilimia 7 mwaka 2003/4 hadi asilimia 4.7 mwaka 2016/17". Amesema Waziri Ummy.
Aidha, Waziri Ummy amesema kuwa Serikali ya Tanzania kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wa maendeleo ikiwemo PEPFAR inaendelea kupanga mikakati mbalimbali ya kudhibiti maambukizi ya UKIMWI, kutoa huduma na matibabu kwa watu wanaoishi na virusi.
Mbali na hayo Waziri Ummy amedai kuwa Serikali imefanikiwa kutoa huduma za utambuzi na matibabu, huku akisisitiza kuwa dhana ya kwamba UKIMWI ni ugonjwa wa kifo imeisha.
Hata hivyo, Waziri Ummy amesema, kufikia mwezi Septemba mwaka 2019 idadi ya watu waliopima na kujua afya zao imefikia asilimia 77.2 na kati yao asilimia 98 wanaendelea na huduma za VVU pamoja na matumizi ya ARV.
Kwa upande wake Balozi wa Marekani nchini Dr. Inmi Patterson amesema Serikali ya Marekani itaendelea kushirikiana na Serikali ya Tanzania katika mapambano dhidi ugonjwa wa UKIMWI na ameipongeza Serikali kupitia Wizara ya Afya kwa jitihada kubwa inazofanya kwa kushirikiana na wadau mbalimbali katika kudhibiti maambukizi na kutoa huduma bora za VVU kwa watu waliogundulika na maambukizi.
Mkutano huo ulijumuisha wadau mbalimbali akiwemo mwakilishi wa Shirika la Afya duniani nchini Tanzania Dkt. Tigest Ketsela pamoja na wataalam kutoka Wizara ya Afya wakiongozwa na Mkurugenzi wa kinga Dkt. Leonard Subi, Ofisi ya Rais TAMISEMI, Tume ya kudhibiti na kupambana na UKIMWI (TACAIDS) pamoja na wadau mbalimbali.
from MPEKUZI
Comments
Post a Comment