Dr Gwajima: Tusimhujumu Rais, Komesheni Ubadhirifu wa Dawa

Na Atley Kuni- TAMISEMI.
Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Dkt. Dorothy Gwajima, amewataka Wafamasia wa Mikoa kote nchini kupambana na kukomesha watu wanaofanya ubadhilifu wa dawa zinazotolewa na serikali kwenda kwenye sehemu za kutolea huduma za afya sambamba na kutafsiri falsafa ya hapa kazi tu kwa vitendo.

Akizungumza katika kikao kazi cha wataalam hao kinachofanyika mjini Dodoma, alisema Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli ametekeleza vema ilani ya Chama cha Mapinduzi kwakuijali na kuipa kipaumbele sekta ya afya na ndio maana katika mwaka wa fedha 2019/20 serikali imepitisha bajeti ya Shilingi bilioni 57.4 ambapo katika mgawanyo eneo la dawa ni miongoni mwa vipaumbele vitatu vilivyo pewa umuhimu.

“Sasa tusimhujumu Mhe. Rais ambaye ameshafanya kazi kubwa na sisi tuliomo ndani ambao tumewekwa kusimamia tunaujuzi na utaalam sehemu ambayo yeye hawezi kuingia, watu wanaiba dawa tunawaangalia, wanaiba vitendanishi tunawaangalia, tutakuwa hatutimizi wajibu wetu kama matazamia yake naya wanachi yanavyotaka” alisema Gwajima.

Gwajima amewataka Wafamasia hao kutumia mfumo wa Ugavi wa dawa wa (elmis) ambao kimsingi taarifa zote za dawa zinaingizwa na kutumika kama muhtadha wa kuombea dawa kwa kila robo. Alisema mfamasia wa Mkoa atakuwa na wajibu wa kuhalalisha maombi ya dawa kwenda MSD kila mara, huku akiitaja mikoa ya kuanzia katika zoezi hilo ni pamoja na Singida, Dodoma, Manyara, Kagera na Geita.

“Tunataka kufanyika kwa Medicine Audit kila robo na taarifa yake kwa kila mkoa iwasilishwe OR-TAMISEMI” alisema Gwajima na kuongeza kuwa “lengo ni kuchakata taarifa za mifumo ya dawa ili kubaini kama kuna hazina ya dawa za kutosha au lah, ili kuweza kusaidia maeneo ambayo yanaupungufu wa dawa.” Alisisitiza Gwajima.

Katika hatua nyingine Gwajima alisema Serikali hivi sasa ipo katika maboresho makubwa ya mfumo wa uendeshaji wa shughuli za Afya (Government of Tanzania Health Management Information System-GoTHOMIS) ambao baada ya kukamilika kwake mfumo utatoa taarifa nyingi za makusanyo ya fedha za dawa mpaka ngazi ya mtumiaji wa mwisho.

Awali kabla yakumkaribisha Mgeni Rasmi, Mkurugenzi wa Idara ya Afya na Ustawi wa Jamii OR-TAMISEMI, Dkt. Ntuli Kapologwe, alisema Sekta ya Afya imekuwa miongoni mwa sekta zilizo pewa kipaumbele na Mhe. Rais hivyo kama wataalam lazima tuoneshe kwa vitendo kuwa Mhe. Rais hajakosea katika hili.

“Mtakumbuka ziara ya mwanzo kabisa Mhe. Rais, alijielekeza katika sekata hii muhimu kwa mustakabali wa maendeleo nchi hasa wakati huu tunapoelekea katika uchumi wa kati ifikapo 2025. Lakini hakuishia hapo toka ameingia madarakani imeendelea kutenga fedha kwaajili ya kujenga na kukarabati vituo vya kutolea huduma za afya, ambapo katika mwaka wa fedha 2017/18 vituo vya afya 352 zikiwepo Hospitali 9, Vituo vya Afya 304 na Zahanati 39 zilikarabatiwa, lakini hivi sasa vituo vinavyo jengwa na kukarabatiwa vimefikia 470 zikiwemo hospitali 67 mpya za Halmashauri ambazo zitakuwa na idara kamili ya dawa” alisema Kapologwe.

Kikao cha Wafamasia kimetayarishwa na Ofisi ya Rais TAMISEMI kwa ushirikiano na wadau wa maendeleo, lengo likiwa nikuweka mipango ya kuhakikisha mianya ya ubadhilifu wa dawa inakomeshwa lakini pia kuweka mikakati endelevu ya upatikanaji wa dawa katika sehemu zote za kutolea huduma za afya.


from MPEKUZI

Comments