Waziri wa Maji Asitisha Vibali vya Ujenzi wa Miradi kwa Wakandarasi kwa Kukosa Uadilifu

Waziri wa Maji, Profesa Makame Mbarawa amesema kuanzia sasa amesitisha kutoa vibali vya ujenzi wa miradi ya maji kwa wakandarasi kutokana na wengi wao kuwa wadanganyifu katika makadirio ya gharama za utekelezaji wa miradi hiyo na kuisababishia Serikali mzigo mkubwa na kukwama kwa miradi mingi katika maeneo mbalimbali nchini.

Kauli imekuja akiwa ziarani mkoani Lindi akitembelea na kukagua ujenzi wa miradi ya maji katika Manispaa ya Mji wa Lindi na Halmashauri ya Wilaya ya Lindi katika kuhakikisha utekelezaji wa miradi hiyo inaenda kwa kasi na kukamilika kwa wakati.

Profesa Mbarawa amesema baada ya kutembelea miradi mingi ya maji amegundua tabia ya wakandarasi wengi wasio waadilifu kuweka gharama kubwa ili kupata faida kubwa, na kumfanya kuchukua uamuzi wa kusitisha vibali vya ujenzi kwa wakandarasi na kutoa kazi hizo kwa Wakala wa Usambazaji Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) pamoja na Mamlaka za Maji.

Akifafanua kuwa maamuzi hayo yamelenga kukomesha tabia hiyo ya wizi wa fedha za Serikali na kuokoa fedha nyingi zinazoweza kutumika katika utekelezaji wa miradi katika maeneo mengine mengi na pia kuipa nafasi Serikali kukamilisha ujenzi wa miradi yake kwa wakati.

Katika hatua nyingine, Profesa Mbarawa amemtaka Mkurugenzi wa Manispaa ya Lindi na Mkandarasi wa Kampuni ya M/S Halem Construction Co. Ltd wakae chini na kufikia makubaliano ya kuiacha Wizara ya Maji ifanye utaratibu wa manunuzi ya bomba za kusambaza maji kwa ajili ya Mradi wa Maji wa Nandambi kwa dhumuni la kuhakikisha unakamilika kwa wakati kutokana na mkandarasi huyo kusuasua.

Profesa Mbarawa amesema fedha za ununuzi wa mabomba hayo zipo na ndani ya wiki mbili mabomba yatakuwa yamefika site kwa ajili ya kukamilisha mradi huo unaotakiwa kukamilika mwishoni wa mwezi Septemba, 2019 kwa gharama ya Shilingi milioni 825.

Aidha, wakazi wa Kijiji cha Nandambi wamweleza Waziri wa Maji, Prof. Mbarawa kuwa hatua hiyo itakuwa na msaada mkubwa kwao ikizingatiwa kuwa mradi huo ulioanza utekelezaji wake Agosti, 2018 na unatakiwa kukamilika mwezi Septemba, 2019 bado mkandarasi hatoi matumaini ya kukamilisha mradi huo kwa asilimia 100 pamoja na ujenzi wa tenki kuwa umekamilika.

Wakati huo huo, Kaimu Mkuu wa Mkoa ya Lindi, Shaibu Ndemanga amesema Serikali ya Mkoa wa Lindi itahakikisha mazungumzo hayo yanafanyika pasipo kupoteza muda ili hatua iliyobaki ikamilike na wananchi wa Nandambi wanufaike na maji.


from MPEKUZI

Comments