Masoko Ya Mazao Kuinua Sekta Ya Kilimo

Na Ismail Ngayonga,MAELEZO
RIPOTI ya Shirika la Kilimo Duniani (FAO) inasema mahitaji ya bidhaa za kilimo yanatarajiwa kukua kwa asilimia 15 katika kipindi cha muongo mmoja ujao huku, ukuaji wa uzalishaji wa bidhaa za kilimo ukitarajiwa kuongezeka kwa kasi zaidi na kusababisha mfumuko wa bei.

Aidha ripoti hiyo iliyotolewa  mwezi Julai mwaka huu inatoa utafiti unaolenga mwelekeo wa miaka kumi ijayo katika soko la bidhaa za kilimo na samaki katika viwango vya kitaifa, kikanda na kimataifa.

Katika ripoti hiyo inaelezwa kuwa miongoni mwa changamoto kubwa inayowakabili wakulima katika Mataifa yanayoendelea ikiwemo Tanzania ni pamoja na ukosefu wa masoko ya mazao yao ndani na nje ya nchi.

Changamoto hiyo imekuwa ikiwakwaza sana wakulima katika miaka ya nyuma wakulima kiasi cha baadhi ya wakulima wa baadhi ya mazao kadhaa kuamua kuachana kabisa na uzalishaji wa mazao husika ikiwemo zao la kahawa na korosho.

Changamoto za wakulima kukosa masoko haziwaathiri wakulima pekee, bali hata serikali hivyo ni suala linalogusa pande zote, kwa sababu serikali nayo inategemea kupata mapato kutokana na usafirishaji wa mazao nje.

Hata hivyo, matumaini yameanza kuonekana kutokana na hatua kadhaa ambazo zinachukuliwa na Serikali ya Awamu ya Tano katika kuboresha sekta ya kilimo ikiwemo kuhimiza uongezaji wa thamani ya mazao na kuweka bei elekezi ya mazao, ambayo inampa motisha mkulima.

Akiwasilisha Hotuba ya Makadirio ya Bajeti ya Mapato na Matumizi kwa mwaka 2019/2020, Waziri wa Kilimo, Japhet Hasunga anasema Wizara kwa kushirikiana na Wizara ya Viwanda na Biashara imeendelea kutekeleza mipango na mikakati ya kupata masoko na kuongeza thamani ya mazao ya kilimo.

Waziri Hasunga anasema Ili kuongeza juhudi zaidi za utafutaji wa masoko ya mazao ya kilimo, Wizara katika mwaka 2018/2019, imeanzisha kitengo cha masoko ya mazao ya kilimo ambacho kitahusika na kutafuta masoko ndani na nje ya nchi na kufanya utafiti na uchambuzi wa kina wa mahitaji ya mazao na bidhaa za kilimo.

“Wizara pia iliboresha mifumo ya masoko ya mazao ya kimkakati kwa kufanya utafiti wa mahitaji ya masoko na kuimarisha vyama vya ushirika, kusimamia mikataba baina ya wanunuzi na wakulima” anasema Waziri Hasunga.

Anaongeza kuwa matokeo ya awali ya utekelezaji ya mifumo hiyo, yameonesha kuwepo kwa tija kwa mkulima, bei nzuri, takwimu na ubora wa mazao, ambapo bei kwa mazao ya kahawa, korosho na kakao kwa soko la ndani ziliimarika ikilinganishwa na masoko ya nje.

Akitolea mfano Hasunga anasema bei ya kahawa ya Arabika katika soko la dunia ilikuwa ni Dola za Marekani 107.04 ikilinganishwa na Dola 112 katika soko la ndani kwa gunia la kilo 50, bei ya kahawa ya Robusta katika soko la dunia ilikuwa Dola 73.90 ikilinganishwa na Dola 87.13 katika soko la ndani kwa gunia la kilo 50.

Akifafanua zaidi anasema Serikali pia imeendelea kutafuta masoko ya zao la muhogo ikiwemo kuingia Makubalino ya Itifaki ya Usafi baina ya Tanzania na Serikali ya China kuwezesha kuuza zao hilo nchini China.

“Hadi mwezi Machi 2019, kampuni tano za Dar Canton Investment, Jielong Holdings (T) Company, EPOCH Agriculture Development, Gelimesha Company na Tanzania Export Processing Zone (TAEPZ) zimesajiliwa kwa ajili ya kuuza muhogo nchini China” anasema Waziri Hasunga.

Hasunga anasema katika mwaka 2018/ 2019, Bodi ya Nafaka na Mazao Mchanganyiko ilipanga kununua tani 14,000 za mahindi na tani 6,000 za mbegu za alizeti, ambapo hadi kufikia Machi 2019, Bodi imenunua mahindi tani 7,230 na alizeti tani 621 na kusaga tani 1,003.0 za mahindi ambazo zimetoa tani 802.4 za unga wa mahindi na tani 208.9 za pumba.

Kwa mujibu wa Hasunga anasema Tani 1,003.0 za unga wa mahindi zenye thamani ya Shilingi 561,680,000 na tani 208.9 za pumba zenye thamani ya Shilingi 45,570,000 ziliuzwa katika mikoa ya Iringa, Mwanza, Dodoma na Dar es Salaam.

Waziri Hasunga anasema ili kujiimarisha zaidi, Bodi imefunga mashine za kukamua mafuta ya alizeti na kusaga mahindi katika eneo la Kizota Jijini Dodoma hadi Machi, 2019 ufungaji wa mashine za kusaga mahindi umefikia asilimia 90 na alizeti asilimia 65.

Mkakati wa Serikali wa kuimarisha masoko ya mazao ni muhimu na wenye tija kwa sababu unalenga kuwatafutia wakulima ufumbuzi wa kero yao ya muda mrefu ya masoko, ambayo pia imekuwa ikisababisha serikali isinufaike zaidi na pato

Aidha masoko ya mazao pia yatasaidia kuchochea kasi ya ukuaji wa viwanda ambavyo Tanzania imepania kuvijenga katika wakati huu wa kuelekea uchumi wa kati ifikapo mwaka 2025.


from MPEKUZI

Comments