Uwepo wa makundi yasiyo na tija, kutegeana katika kazi na kutoshirikiana baina ya watumishi kumesababisha miradi ya maendeleo inayotekelezwa katika halmashauri ya Wilaya ya Momba kuchelewa kukamilika.
Hayo yamebainishwa jana na baadhi ya watumishi wa Halmashauri hiyo walipokuwa wakizungumza na Mkuu wa Mkoa wa Songwe Brig. Jen. Nicodemus Mwangela alipokutana nao kutaka kufahamu sababu za kutokamilika kwa wakati ujenzi wa miradi mbalimbali katika halmashauri hiyo.
Mmoja wa watumishi amesema, “unapokuwa na mradi wa sekta fulani mfano afya, kilimo au elimu watumishi wenzako wanakaa pembeni hawakusaidii, ni kama wanakutegea waone utakavyoshindwa kitu ambacho sio sahihi, miradi yote ni ya halmashauri na inalenga kuwanufaisha wananchi wote.”
Watumishi hao wamesema baada ya kuzungumza na Mkuu wa Mkoa wameona kuwa makundi na kutoshirikiana havitaijenga halmashauri na hivyo wameapa kubadilika na kufanya kazi kwa pamoja kama timu moja.
Aidha Mkuu wa Mkoa wa Songwe Brig. Jen. Nicodemus Mwangela amesema anaamini tatizo la kutoshirikiana baina ya watumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Momba limeisha na watafanya kazi kwa pamoja.
Brig. Jen. Mwangela ameongeza kuwa mara baada ya kikao hicho ameona ushirikiano wa watumishi katika ujenzi wa Soko la Mazao la Kakozi ambapo wote kwa pamoja wameonyesha nia kufanikisha ujenzi huo kwakuwa umesha chelewa kwa zaidi ya miezi sita.
Naye Msimamizi wa Ujenzi wa soko la mazao la Kakozi Aloyce Sakaya amesema kwa sasa mradi huo utatekelezwa kwa kasi zaidi kwakuwa changamoto zilizo sababisha ukachelewa ikiwa ni pamoja na kutoshirikiana baina yao zimeondolewa.
from MPEKUZI
Comments
Post a Comment