Katibu Mkuu wizara ya afya Dkt.Chaula Ahitimisha Kongamano La Tatu La Kutathimini Masuala Ya Afya Nchini.

Na.Faustine Gimu Galafoni,Dodoma.
Katibu Mkuu  wizara ya afya , Maendeleo ya jamii,jinsia,Wazee na watoto Dkt Zainabu Chaula amefunga kongamano la tatu la mwaka la kufuatilia na kutathmini masuala ya afya Nchini.

Akizungumza katika Kongamano hilo Septemba 25,2019   jijini Dodoma  ,Dkt Chaula amesisitiza juu ya matumizi ya takwimu kwa wadau wa afya ili iwasaidie katika upataji wa taarifa sahihi.

Awali Akitoa taarifa fupi mbele ya Mgeni Rasmi yenye tathmini ya mafunzo ikiwa na mjumuisho wa kongamano la pili lililofanyika mwaka jana na la tatu mwaka huu, kaimu mkuu wa shule ya utawala na Management ya chuo kikuu cha Mzumbe Dkt Eliza Mwakasangula amesema tafiti zifanyike na kuleta majibu juu ya namna bora ya kuimarisha na kujenga mifumo ya kuchakata taarifa za  huduma za afya nchini.

Katika hatua nyingine Dkt Eliza amesema vituo vya afya kumiliki miradi na taarifa kwa matumizi yao wenyewe ni chachu kuu ya kuboresha taarifa zinazokusanywa na kuzitumia katika kufanya maamuzi.

Mbali na hilo Dkt eliza amesema kuwe na ushirikiano baina ya wizara na vyuo vya ndani na nje ya nchi kuendelea kuchapisha na kuwasilisha matokeo ya tafiti zinazofanyika kwa wahusika  ili waweze kutumia matokeo ya tafiti hizo kwa kuboresha huduma ya afya Tanzania.

Akizungumza kwa niaba ya washiriki walioshiriki katika kongamano hilo Joseph Bura amesema maelekezo yote yaliyotolewa katika kongamano hilo watakwenda kuyafanyia kazi kama inavyotakiwa.
 
Kongamano hilo  la kutathimini na kufuatilia masuala ya Afya nchini limeandaliwa na chuo kikuu cha Mzumbe kwa kushirikiana na chuo cha St Fransisco Nchini Marekani na kushirikisha wadau mbalimbali  kwa lengo la kufuatilia na kutathimini masuala ya afya.


from MPEKUZI

Comments