WAZIRI MKUU, Kassim Majaliwa amewakaribisha wafanyabiashara na wawekezaji kutoka nchini Mauritius waje washirikiane na Watanzania katika uwekezaji kwenye maeneo mbalimbali yakiwemo ya utalii, viwanda vya sukari, nguo na bidhaa za uvuvi.
Ametoa kauli hiyo leo, (Jumatano, Agosti 28, 2019) wakati alipokutana na kufanya mazungumzo na Waziri Mkuu wa Mauritius, Pravind Kumar katika Ukumbi wa Monyesho wa Pasfico Yokohama nchini Japan.
Waziri Mkuu amesema nchi ya Mauritius ina uwezo mkubwa sana katika uzalishaji wa sukari na wanayo nafasi kubwa ya kushirikiana na Watanzania katika kilimo cha miwa na ujenzi wa viwanda vya sukari na Tanzania ina ardhi nzuri na kubwa inayofaa kwa kilimo hicho pamoja na soko kubwa ndani na nje ya nchi.
Amesema uwekezaji katika sekta ya sukari utasaidia kuunga mkono juhudi za Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Rais Dkt. John Magufuli za kuhakikisha inamaliza tatizo la upungufu wa sukari nchini.
Akizungumzia kuhusu sekta ya utalii, Waziri Mkuu amesema Mauritius imefanya vizuri sana katika utalii na hasa ule wa kutumia fukwe za bahari. “Kwa vile Tanzania inazo fukwe za bahari na maziwa naamini ushirkiano katika eneo hilo utatuletea tija.”
Kuhusu usafiri wa anga, Waziri Mkuu amesema kuwa wakati umefika sasa kwa Shirika la Ndege la Tanzania (ATCL) kuanza safari za kwenda Mauritius ili kuvutia watalii wengi wanaokwenda Mauritius kufanya utalii wa fukweni waje pia nchini.
Kuhusu viwanda vya nguo, Waziri Mkuu amewahamasisha wafanyabiashara wa Mauritius kuwekeza nchini hasa katika viwanda vya nyuzi za pamba na nguo kwani Tanzania hivi sasa inazalisha pamba nyingi na yenye ubora wa juu.
“Watanzania wengi wameishia kuwekeza kwenye viwanda vya kuchambua pamba hivyo wanalazimika kuuza pamba yao nje ya nchi na wenzetu Mauritius wameenda mbali zaidi kwani wana viwanda vya nguo na viwanda vya nyuzi. Kwa sasa Serikali ya Tanzania imeweka mkakati wa kujenda viwanda vya nguo ili kuongeza tija.”
Amesema kwa sasa wamekuabaliana na Waziri wa Mkuu huyo wa Mauritius kuwakutanisha Mawaziri wa viwanda na Biashara wa Mauritius na Tanzania wakae pamoja kwa ajili ya kufanya mazungumzo yenye lengo la kuwashawishi wafanyabiashara wa Mauritius waje wawekeze katika viwanda vya nguo na nyuzi nchini.
Kadhalika,Waziri Mkuu amezungumzia kuhusu sekta ya Uvuvi, ambapo amesema Tanzania ina eneo kubwa la bahari na maziwa linalofaa kwa uvuvi wa kibiahara na lina samaki wengi lakini wanavuliwa kwa kiwango kidogo sana kutokana na uwekezaji duni katika sekta hiyo.
Amesema ingawa Serikali ya Awamu ya Tano inaandaa mazingira ya kufufa kampuni za uvuvi nchini, bado nafasi ipo kwa wawekezaji kutoka nje ya nchi hasa nchini Mauritius kuja Tanzania kuwekeza kwenye uvuvi.
Kwa upande wake, Waziri Mkuu wa Mauritius, Pravind ameihakikishia Serikali ya Tanzania kuwa nchi yake iko tayari kufanya mazungumzo na Wizara na Taasisi zinazohusika na masuala ya uwekezaji nchini ili kupata taarifa za kutosha zitakazomwezesha kuwashawishi wafanyabiashara wa nchi yake waje wawekeze nchini.
Mazungumzo hayo pia yalihudhuriwa na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikikiano wa Afrika ya Mashariki, Profesa Paramagamba Kabudi na viongozi kutoka Serikali ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.
(mwisho)
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
JUMATANO, AGOSTI 28, 2019.
from MPEKUZI
Comments
Post a Comment