Polisi Pwani Yakamata Magunia Tisa Ya Bangi

MWAMVUA MWINYI, PWANI
JESHI la Polisi mkoani Pwani linamshikilia dereva Francis Deogratias (30) mkazi wa Mwananyamala Jijini Dar es Salaam kwa tuhuma za kusafirisha bhangi magunia tisa kila moja likiwa na uzito wa kilo 50.

Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake mjini Kibaha kamanda wa polisi mkoani humo Wankyo Nyigesa alisema kuwa bhangi hiyo ilikutwa kwenye gari alilokuwa akiendesha mtuhumiwa.

Nyigesa alisema kuwa tukio hilo lilitokea Agosti 27 majira ya saa 3:30 usiku eneo la Maili Moja askari wakiwa doria walikamata gari hilo aina ya Toyota Prado yenye namba za usajili T855CYP rangi ya Silver likitokea mkoani Morogoro.

"Mtuhumiwa alikuwa na wenzake watatu ambao walikimbia na msako mkali unaendelea kuwatafuta ili waje wajibu tuhuma zitakazowakabili za kusafirisha bhangi," alisema Nyigesa.

Alisema kuwa watu wanaojishughulisha na uhalifu kwa sasa hawana nafasi na waangalie shughuli halali kwani hawatavumiliwa na hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi yao na wananchi watoe taarifa za uhalifu.


from MPEKUZI

Comments