Miradi ya mamilioni ya TASAF yazinduliwa Njombe

Na Amiri kilagalila-Njombe
Jumla ya miradi mikubwa minne ya jengo la utawala,nyumba za walimu nne na bweni la wanafunzi wa kike yenye thamani ya milioni 320 iliyotekelezwa na mfuko wa maendeleo ya jamii Tanzania TASAF imezinduliwa katika shule ya sekondari Mlowa iliyopo kata ya Mlowa mjini Makambako mkoani Njombe.

Akizungumza na wananchi wakati wa uzinduzi wa miradi hiyo, mkaguzi wa ndani wa Tasaf  Christopher Sanga kwa niaba ya mkurugenzi,amesema miradi hiyo ni miongoni mwa miradi mingi inayotekelezwa kwa sasa kwa mikoa miwili ya Arusha na Njombe licha ya kuwa mradi mkuu ukiwa ni kushughulikia kaya maskini.

“Miradi hii ambayo inazinduliwa hapa ni miongoni mwa miradi mingi inayotekelezwa kwa kipindi hiki katika mikoa yetu miwili ya Arusha na Njombe,mradi mkuu unaoendelea wa Tasaf unajikita katika kushughulikia kaya maskini na huko tunakoenda tutatumia sana neno kaya washiriki katika mpango”alisema Christopher Sanga

Sanga amesema utekelezaji wa miradi hiyo ni mpango muunganiko ndani ya mpango mkubwa unaotekelezwa na mfuko wa jamii Tanzania.

“Miradi hii iliyotekelezwa hapa ni mpango muunganiko ulioletwa ndani ya mpango mkubwa wa Tasaf unaotekelezwa na serikali ambayo serikali inatafuta vyanzo vya fedha na chanzo cha fedha cha miradi hii inatoka katika nchi za wazalishaji wa mafuta kwa wingi inaitwa OPEC kwa hiyo hii ni awamu ya tatu kwa kutekeleza huku awamu ya kwanza na ya pili ilitekelezwa katika mikoa ya Mtwara na Lindi”aliongeza Sanga

Katika hatua nyingine Sanga amewapongeza wananchi wa kijiji cha Mlowa kwa kushirikiana na uongozi wa kijiji hicho kwa kuwa upatikanaji wa miradi hiyo umetokana na utekelezaji wa ufanisi wa mradi wa kwanza wa hosteli ya wasichana.

Naye mkuu wa mkoa wa Njombe Christopher Olesendeka ambaye ndiye mgeni rasmi katika uzinduzi huo,ametoa shukrani kwa Rais Magufuli kuwasaidia wananchi wa kata hiyo kupitia mfuko wa Tasaf na kutoa wito kwa wananchi kuendelea kuunga mkono serikali katika kuleta maendeleo.

“Wazee hawa wamepewa dhamana ya kusimamia mfuko huu wa maendeleo ya jamii ulio chini ya mfuko wa Rais,kwa hiyo mkiona fedha hizi zinaletwa kwenu maana yake zimetafutwa na Rais wa jamhuri ya muungano wa Tanzania,tunachopaswa ni kuendelea kuunga mkono jitihada za Rais Magufuli,lakini binafsi pia nimefarijika na haya majengo yote yalivyojengwa kwa viwango”alisema Olesendeka

Baadhi ya wananchi wa kata hiyo wametoa shukrani zao kwa mfuko huo kutokana na kuwaunga mkono katika maendeleo ya shule yao huku wanafunzi wa shule hiyo wakiahidi kutoa zawadi ya kupanda kitaaluma na kuomba mfuko huo kuwasaidia ujenzi wa bwalo kwa ajili ya chakula,jiko na bweni la wavulana.


from MPEKUZI

Comments