Anayedaiwa kumuua na kumchoma mkewe Kwa Magunia Mawili ya Mkaa Aomba Apatiwe Simu Zake Ili Ahamishe Fedha Zake

Mshtakiwa Hamisi Luwongo anayetuhumiwa kumuua mkewe Naomi Marijani kisha kumchoma na magunia mawili ya mkaa, ameomba apewe laini  zake mbili  za simu zenye zaidi ya Sh milioni tano ili awape ndugu zake wakamlipie mwanawe ada.

Mshtakiwa huyo amedai hayo leo Jumanne Agosti 27, katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu mbele ya Hakimu Mkazi, Salum Ally, wakati kesi hiyo ilipotajwa.

Wakili wa Serikali Mwandamizi, Wankyo Simon amedai upelelezi haujakamilika akaomba kesi iahirishwe.

“Kesi imekuja kwa ajili ya kutajwa na upelelezi wake bado haujakamilika hivyo tunaomba tarehe nyingine kwa ajili ya kutajwa,” amedai Simon.

Wakili Simon baada ya kueleza hayo, mshtakiwa alinyoosha mkono na kumueleza hakimu kuwa ana mambo mawili anataka kuyasema ambayo ni   nakala yake ya hati ya mashtaka na laini zake za simu.

Aliomba apatiwe laini hizo kusaidia familia yake na ada na kusisitiza kuwa katika kituo hicho kuna simu zake nne, mbili ndio zenye kiasi hicho cha fedha. 

 
“Mheshimiwa Kituo Kikuu cha Polisi (Central) kuna simu zangu nne lakini katika hizo simu kuna laini mbili ya Tigo na Airtel, zina zaidi ya Sh milioni tano, naomba simu ziletwe mahakamani nihamishie hizo fedha kwa ndugu yangu zikasaidie kumlipia mwanangu ada,” amedai.

Hata hivyo, wakili Simon amedai hawawezi kumpatia laini hizo kwa kuwa simu zake ni sehemu ya ushahidi wa kesi hiyo.

Amesema kama anahitaji fedha hizo aandike barua ya malalamiko na kuipeleka kwa Mkurugenzi wa Mashtaka Tanzania ( DPP) na nakala  aipeleke kwa Mkurugenzi wa Makosa ya Jinai nchini( DCI) huku hakimu Ally akimtaka mshtakiwa kufanya kile  alichoelezwa na upande wa mashtaka.

Baada ya kueleza hayo kesi hiyo iliahirishwa hadi Septemba 10, 2019 itakapotajwa tena huku mshtakiwa akirudishwa mahabusu.


from MPEKUZI

Comments