Tudu Lissu Kasema Kwa Sasa Kapona, Hatumii Tena Dawa wala Magongo

Mwanasheria Mkuu wa chama kikuu cha upinzani nchini Tanzania cha Chadema, Tundu Lissu amesema amehitimisha matumizi ya dawa alizoanza kuzitumia tangu Septemba 7 mwaka 2017.

Lissu alianza kutumia dawa hizo Septemba 7 mwaka 2017 baada ya kushambuliwa kwa risasi zaidi ya 30 akiwa katika makazi yake Area D jijini Dodoma ambapo tangu wakati huo amekuwa akipatiwa matibabu nje ya nchi.

Katika salamu kwa marafiki zake alizozitoa leo Jumatano Julai 31, 2019, kupitia ukurasa wake wa Instagram,  Lissu ameandika;

 
Hello Marafiki wa Mimi,
Habari za masiku mengi. Sijawasemesha kwa kitambo kidogo. Nisameheni bure, nafikiri mnafahamu jinsi ambavyo mambo yamekuwa mengi. Nina mambo mawili, nayo ni mema tu. .

La kwanza linahusu hali yangu ya afya. Leo tarehe 31 Julai, 2019, ni siku ya kwanza tangu niliposhambuliwa Septemba 7, 2017, situmii dawa ya aina yoyote. .

Kwa maelekezo ya madaktari wangu, jana ilikuwa siku ya mwisho ya mimi kutumia madawa ambayo nimeyatumia tangu siku niliposhambuliwa. .

Na jana hiyo hiyo nilitimiza mwezi mzima tangu niache kutumia magongo. Ijapokuwa bado nachechemea kwa sababu ya goti kutokukunja sawa sawa, sasa ninatembea bila msaada wa magongo. .

Safari yangu, na yetu, ndefu ya matibabu itakamilika Agosti 20 nitakapokutana na timu ya madaktari wangu kwa ajili ya vipimo vya mwisho na ushauri. .

Baada ya hapo itakuwa ni maandalizi ya kurudi makwetu. Hakutakuwa na sababu tena ya kitabibu ya mimi kuendelea kukaa Ulaya. .

Kwa vile tumekuwa pamoja kwenye safari hii ndefu, hatuna budi kupongezana na kumshukuru Mungu kwa hatua hii nzuri nilikofikia. Mimi na familia yangu hatutachoka kuwashukuru sana kwa kuwa pamoja nasi katika kipindi chote hiki kigumu. Mungu awabariki sana. .

La pili linahusu ubunge wangu. Tangu Spika Ndugai anivue ubunge, sijasema maneno mengi sana, zaidi ya kusema kwamba tutaenda Mahakama Kuu kupinga uamuzi huo. .

Kesi za ubunge, kama zilivyo kesi zote za uchaguzi wa kisiasa, ni kesi za kisiasa. Ni mwendelezo wa mapambano ya kisiasa katika uwanja tofauti. .

Kwa sababu hiyo, ni kesi nyeti na za kipekee sana. Zinahitaji umakini mkubwa katika kuziandaa na kuziendesha. Nina uzoefu mkubwa nazo, kwa sababu nimezifanya sana tangu 2005. 
 
Sasa ninaweza kuwafahamisha kwamba mimi na timu ya mawakili wangu tuko tayari kuingia Mahakama Kuu ya Tanzania. Tutafanya hivyo muda wowote kuanzia leo. Maandalizi yote yanayohitajika yamekamilika.
 
Tunataka kuiomba Mahakama Kuu itoe jibu la swali alilouliza Spika Ndugai na walio nyuma yake: je, Spika wa Bunge la Tanzania ana uwezo kikatiba na kisheria, wa kufuta ubunge wa mbunge yeyote yule, kwa sababu yoyote ile, bila kumuuliza mbunge husika jambo lolote kuhusu sababu za kumfuta ubunge huo??? .

Nitawajulisheni mara moja kesi hii itakaposajiliwa rasmi. Kama itawapendeza, nitawaomba mtakaopata nafasi kuhudhuria mahakamani, kwa niaba yangu, wakati wote kesi hiyo itakapokuwa inaendelea. .

Nilitaka kuwashirikisheni haya kwa leo. Nawashukuruni sana na Mungu awabariki sana.


from MPEKUZI

Comments