Tundu Lissu Kwenda Mahakamani Kupinga Kuvuliwa Ubunge

Baada ya Spika wa Bunge la Tanzania, Job Ndugai kusema Mbunge wa Singida Mashariki (Chadema), Tundu Lissu amepoteza sifa za kuendelea kuwa mbunge, mwanasiasa huyo ambaye anaendelea kuuguza majeraha ya risasi ughaibuni amesema atakwenda mahakamani kupinga uamuzi huo.

Lissu alisema hayo jana Ijumaa Juni 28, 2019 wakati akizungumza na gazeti la Mwananchi  kwa njia ya simu akiwa Ubelgiji, ambapo amesisitiza kuwa, tangu aliposhambuliwa kwa risasi zaidi ya 30 akiwa Area D jijini Dodoma Septemba 7, 2019 amekuwa akipata matibabu nje ya nchi.

Amesema kwa hatua ya sasa, “Nitawasiliana na wanasheria wangu haraka iwezekanavyo ili kuona cha kufanya lakini Septemba 7 (mwaka huu) ambayo nilikwisha kusema nitarudi sitabadili, nitarudi na alichokifanya Ndugai ni kukoleza mjadala.”

Jana Ijumaa, Spika Ndugai aliliambia Bunge hilo kuwa amewandikia Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi kumjulisha kuwa kiti cha ubunge wa Singida Mashariki kipo wazi.

Amesema hatua hiyo inatokana na Lissu kutojaza taarifa za mali na madeni na sababu ya pili kutokutoa taarifa kwa Spika mahali alipo.

Mara baada ya kushambuliwa kwa risasi Septemba 7 mwaka 2017 jijini Dodoma, mwanasiasa huyo  alipelekwa Hospitali ya Rufaa ya Dodoma na usiku wa siku hiyo akahamishiwa hospitali ya Nairobi nchini Kenya ambapo alipatiwa matibabu hadi Januari 6, mwaka jana na kisha kuhamishiwa nchini Ubelgiji hadi leo.


from MPEKUZI

Comments