Askari wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), MT 77341 Johanes Kubambi, amepandishwa kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kinondoni, Dar es Salaam na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Tanzania (Takukuru) kwa shtaka la kuomba rushwa ya Sh 700,000.
Akisoma hati ya mashtaka mbele ya Hakimu Karoline Kiliwa, Wakili wa Takukuru, Vera Ndeoya, alidai kuwa katika ofisi za jeshi la akiba, Wilaya ya Kinondoni, mshtakiwa aliomba rushwa kwa Kelvin Fabian ili aweze kumpatia nafasi ya mafunzo ya jeshi.
Mshtakiwa alikana kutenda kosa hilo na Ndeoya alidai upelelezi wa kesi hiyo bado haujakamilika, hivyo aliiomba mahakama kutaja tarehe nyingine.
Hata hivyo, Hakimu Kiliwa alisema dhamana ipo wazi kwa mshtakiwa kuwa na wadhamini wawili ambao sio wanajeshi wala polisi na wawe na barua zinazotambulika kisheria, watakaotoa bondi ya Sh milioni 1 kila mmoja.
Mshtakiwa alishindwa kukidhi masharti ya dhamana na kurudishwa rumande hadi Juni 28 kwa ajilii ya kutimiza masharti ya dhamana.
from MPEKUZI
Comments
Post a Comment