Waziri Kabudi: Hatuwezi Kupiga Magoti Kuomba Misaada

Waziri wa Mambo ya Nje, Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Profesa Palamagamba Kabudi amesema Tanzania haikupiga magoti katika kipindi cha utawala wa Awamu ya pili chini ya Ali Hassan Mwinyi, ilipokuwa na hali ngumu, hivyo haiwezi kufanya wakati huu ikiwa na hali nzuri zaidi.

Profesa Kabudi aliliambia Bunge jana jioni alipokuwa akijibu hoja za wabunge waliochangia mjada wa bajeti ya wizara kwa mwaka wa fedha wa 2019/2020.

Alisema licha nchi kutokuwa na akiba ya kutosha ya fedha za kigeni wakati huo wa Awamu ya pili (1985-1995), Tanzania haikupiga magoti kuomba msaada lakini sasa, Taifa lina akiba ya fedha za kigeni za miezi mitano.

“Kama tuliweza kwa wakati huo hatuwezi kushindwa katika awamu hii ya (Rais John) Magufuli. Tumeamua kujitegemea,” alisema Kabudi.

Profesa Kabudi alisema Tanzania ndiyo nchi pekee Afrika ambayo haijawahi kushindwa vita na ndiyo nchi iliyowarudisha wapigania uhuru katika nchi zao.

Alisema ndani ya Tanzania kuna watu aliowaita mabarakuli ndani ya nchi wanaofanya kazi za vibaraka wa kubeza juhudi za Serikali wanapoona mafanikio.

Alisema hiki ndicho kizazi cha mwisho kwa fedheha lakini kwa wajukuu wanaokuja hawatakiwi kuona fedheha hiyo.


from MPEKUZI

Comments