Ofisa madini Mkazi wa Mkoa wa kimadini wa Simanjiro, Daudi Ntalima amewapa miezi sita wamiliki na wachimbaji wa madini ya Tanzanite Mji mdogo wa Mirerani, kuboresha miundombinu ya migodi yao la sivyo itafutiwa leseni.
Ntalima aliyasema hayo wakati akizungumza kwenye kikao kazi na mameneja, wachimbaji na wamiliki wa migodi ya Tanzanite Mji mdogo wa Mirerani.
Alisema ametoa miezi sita hadi mwezi Septemba kwani ikifika mwezi Octoba wataanza kuchukua hatua na wanaanza kuhesabu miezi sita hiyo kuanzia mwezi Aprili hadi Septemba.
Alisema hawezi kutoa muda wa mwaka mmoja kwani ni muda mrefu hivyo wamiliki wa migodi hiyo zaidi ya 800 wajitahidi kuboresha miundombinu yao kabla ya miezi sita kumalizika.
“Migodi yote inapaswa kuwekewa uzio wa ukuta wa matofali au mabati ili kuimarisha ulinzi na usalama mgodini na siyo senyenge mmiliki akishindwa hilo mgodi utafutiwa leseni,” alisema Ntalima.
Mwenyekiti wa chama cha wachimbaji madini mkoani Manyara (Marema) Tawi la Mirerani, Shwaibu Mushi alisema wachimbaji hao wanaiomba Serikali kuwapa muda mwaka mmoja ili waboreshe miundombinu ya migodi yao ikiwemo kuweka uzio.
Mushi alisema wengi wao uchumi wao ni mdogo hivyo wanaomba muda huo ili kutekeleza hilo kwani agizo hilo limekuja kipindi ambacho wengi wao wana hali ngumu.
“Wachimbaji wadogo bado wanahitaji kuwa wachimbaji wakubwa baada ya kupata madini, tuliomba tuongezewe muda wa mwaka mmoja ili tutekeleze hilo japo tunashukuru kwa kutuongezea miezi sita,” alisema.
Mwenyekiti wa kamati ya Tanzanite, Money Yousuph alisema wachimbaji wamegawanyika kwenye matabaka tofauti kiuchumi hivyo wanaomba mwaka mmoja wa kutekeleza hilo.
“Ofisa madini mkazi Ntalima wewe ni mlezi wetu na mchimbaji asiyekuwa rasmi mnamtambua na hamchukulii hatua kali na pia ukuta siyo kero ni tija tunaomba busara na hekima zako kwani sisi ni wasikivu,” alisema Yousuph.
from MPEKUZI
Comments
Post a Comment