Serikali imezindua mpango wa matumizi bora ya ardhi kwa vijiji, wilaya na mikoa itakayopitiwa na Mradi wa Bomba la Mafuta Ghafi la Afrika Mashariki (EACOP), ikiwa ni hatua nyingine katika utekelezaji wa mradi huo.
Mpango huo umezinduliwa katika Kijiji cha Sojo wilayani Nzega mkoani Tabora juzi na Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi aliyeambatana na Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu pamoja na Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Aggrey Mwanry na Meneja Mradi wa EACOP, Mantin Tiffen.
Akizungumza na wananchi wa Sojo, Waziri Lukuvi alisema mpango huo wa matumizi ya ardhi unahusisha mikoa nane, wilaya 24 na vijiji 226 ambapo vijiji 30 vipo katika Mkoa wa Tabora.
“Mpango huu unazinduliwa katika Kijiji cha Sojo kwa niaba ya vijiji vyote nchini kwa kuwa hapa Sojo ndipo patakuwa na kituo kikubwa cha kutoa huduma katika mradi wa bomba la mafuta kuliko vituo vingine, kwani kutakuwa na kambi kuu na kiwanda cha kutayarisha mabomba yatakayotumika kusafirisha mafuta kitajengwa hapa,” alisema Lukuvi.
Katika hatua nyingine, Waziri Lukuvi alitoa onyo kwa wavamizi wa ardhi iliyotengwa kwa ajili ya mradi huo kuwa tayari mkuza wote ulishapigwa picha za anga, hivyo fidia itatolewa kwa wananchi wanaostahili tu.
Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu, alisema kazi za mradi wa EACOP zilizopangwa kufanyika katika kijiji hicho, zina uwekezaji wa Sh bilioni 600 na matarajio ni kuwa kazi hizo zitaanza Septemba mwaka huu.
Alisema kutakuwa na ajira zitakazozalishwa, hivyo alitoa wito kwa wananchi kuchangamkia fursa zitakazojitokeza kutokana na uwekezaji huo.
“Mpaka sasa mradi wa Bomba la Mafuta Ghafi umeshatoa ajira zaidi ya 200 na matarajio ni kuwa utaendelea kutoa ajira zaidi kwa Watanzania,” alisema Mgalu.
Kuhusu umeme, alieleza kuwa Wizara iko katika mpango wa kusambaza umeme kwenye vijiji vyote vinavyopitiwa na mkuza huo kwa gharama ya Shilingi elfu 27,000 tu ili kuweka mazingira wezeshi ya kutekeleza mradi husika.
from MPEKUZI
Comments
Post a Comment