Serikali Kuendelea Kutatua Changamoto Za Wawekezaji Nchini.

Serikali imedhamiria kuendelea kutatua changamoto zinazowakabili wawekezaji nchini ili kuhakikisha kunakuwa na mazingira rafiki yatakayowavutia kuwekeza nchini.

Kauli hiyo imetolewa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Uwekezaji Mhe. Angellah Kairuki wakati akifungua mkutano wa wawekezaji wa Uingereza waliopo nchini walipokutana kujadili masuala ya Uwekezaji uliofanyika Mei 29, 2019 katika Ukumbi wa Mikutano wa Coral Beach Jijini Dar es Salaam.

Mkutano huo ulihudhuriwa na Naibu Waziri wa Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Kazi, Vijana na Ajira Mhe.Anthony Mavunde, Balozi wa Uingereza Nchini Mhe.Sarah Cooke pamoja na Mwenyekiti wa Makampuni ya Biashara ya Uingereza Bw.Kalpesh Mehta, viongozi wa makampuni ya uwekezaji nchini, pamoja na baadhi ya viongozi wa Taasisi za Sekta ya Umma na Binafsi.

Akizungumza wakati wa mkutano huo, Waziri Kairuki alieleza lengo la kukutana na wawekezaji kutoka Uingereza ni pamoja na kujadili masuala yote yanayowahusu wawekezaji kwa kuzingatia changamoto zinazowakabili na kuona namna bora ya kuzitatua ili kuendelea kufikia lengo la kuwa na mazingira bora ya biashara na uwekezaji nchini.

“Tumezingati umuhimu wa wawekezaji nchini, hivyo tumekutana hii leo ili kusikiliza kero na changamoto zinazowakabili ili kuona namna bora ya kuboresha mazingira na kutambua fursa zilizopo nchini ili kuendelea kuwekeza nchini”, alisema Waziri Kairuki.

Waziri aliongezea kwamba, kwa kuzingatia kuwa mnamo mwezi Machi mwaka 2019 Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt.John Pombe Magufuli aliutangaza mwaka huu kuwa ni mwaka wa uwekezaji alipokutana na waheshimiwa mabalozi wa nchi za nje ambao wapo nchini ikiwa ni kiashiria cha kufungua mwaka mpya.

Aliongezea kuwa, kwa kuzingatia mchango wa sekta binafsi katika ukuaji wa uchumi ikiwemo ongezeko la ajira hivyo tunapaswa kuzingatia na kuboresha mazingira yatakayochochea kuendelea kuchangia katika uzalishaji wa ajira nyingi nchini.

“Sekta binafsi ndiyo kiini cha ukuaji wa uchumi kwa upande wa kuongeza ajira hivyo tunatambua mchango huo ambapo hadi sasa wawekezaji wa uingereza wamechangia katika ukuaji wa ajira kwa kuzalisha ajira laki tatu,”alisisitiza Waziri Kairuki.

Kwa upande wake Balozi wa Uingereza Nchini Mhe.Sarah Cooke aliipongeza Serikali ya Tanzania kwa kuona umuhimu wa kukutana pamoja kujadili masuala ya uwekezaji na kuendelea kujadili namna ya kuwezesha wawekezaji kutoka uingereza kuendelea kuwa wadau muhimu nchini na kuhakikisha nchi zote mbili zinanufaika.

“Ni kweli tumeenedelea kuwekeza Tanzania kwa kuzingatia mazingira yaliyopo hivyo ni vyema kukawa na maboresho zaidi katika mazingira hayo kwa kuendelea kutatua changamoto zilizopo kwa sasa ili tuendelea kushirikiana pamoja,” alieleza Balozi.Cooke

Aliongezea kuwa nchi ya Uingereza imelenga kuwa kinara cha uwekezaji katika nchi za Afrika hiyo ni wakati sahihi wa kuendelea kutumia fursa zilizopo barani humo ili kufikia malengo.

“Ifikapo mwaka 2022 Nchi yetu imeweka malengo ya kuwa wawekezaji bora barani Afrika hivyo tunaendelea kushirikianana nchi za Afrika ili kuwa na nia moja na kuwa na mahusiano yenye tija hasa katika masuala ya uwekezaji”,alisema Balozi Cooke.

Kwa upande wake Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Kazi, Vijana na Ajira Mhe. Anthony Mavunde alieleza kuwa, Serikali itaendelea kuboresha mazingira ya biashara ili kuchangia ongezeko la ajira kwa vijana wa Kitanzania ili kujikwamua kiuchumi.

Aidha alifafanua kuwa, ili kuendelea kukuza ujuzi kwa vijana na kuondokana na changamoto za ukosefu wa ajira Serikali itaendelea kulinda ajira za watanzania na kuboresha mazingira ya sekta binafsi ambao ni wadau muhimu katika kuzalisha ajira nchini.



from MPEKUZI

Comments