Na Lilian Lundo - MAELEZO, Dodoma.
Baraza la Taifa la Elimu na Ufundi (NACTE) kwa kushirikiana na Vyuo na Taasisi za Elimu na Mafunzo ya Ufundi kwa mara ya kwanza limeandaa Maonesho ya Elimu ya Ufundi na Mafunzo ambayo yamefanyika Jijini Dodoma tarehe 27 hadi 30 Mei, katika uwanja wa Jamhuri.
Maonesho hayo yaliyofanyika kwa takribani siku tano na kufungwa leo na Naibu Waziri wa Elimu Sayansi na Teknolojia, William Ole Nasha ambapo kabla ya hotuba ya kufunga maonesho hayo, Ole Nasha aliweza kujionea shughuli mbalimbali zinazofanywa na Vyuo na Taasisi za Elimu na Mafunzo.
Ole Nasha amesema kuwa, maonesho hayo yametoa fursa kubwa kwa wadau wa Elimu ya Ufundi na Mafunzo ambapo wameweza kujionea shughuli mbalimbali zinazofanywa na Vyuo na Taasisi na Ufundi za Elimu ya Mafunzo na Ufundi. Vile vile kufahamu huduma na bidhaa zinazotolewa na Taasisi hizo.
Vile vile amesema kupitia maonesho hayo Vyuo na Taasisi zilizoshiriki zimeweza kukutana pamoja na wadau hao, hivyo kupata fursa ya kujibu changamoto pamoja na kupokea ushauri kutoka kwa wadau wao.
Aidha amesema, maonesho hayo yametoa fursa kwa wanafunzi na wazazi kufahamu vyuo na masomo wanayotoa pamoja na kupata ushauri wa chuo gani mwanafunzi anaweza kujiunga kutokana na ufaulu wake.
Ole Nasha ameitaka NACTE kuhakikisha maonesho hayo yanafanyika kila mwaka ili wadau wa elimu ya ufundi na mafunzo waendelee kunufaika na kupata uelewa wa shughuli zinazofanywa na vyuo na taasisi za elimu ya ufundi na mafunzo.
Kwa upande wake, Katibu Mtendaji wa NACTE Dkt. Adolf Rutayuga amesema jumla ya Taasisi 100 zimeshiriki maonesho hayo ambapo kati ya Taasisi hizo 71 ni vyuo vya ufundi na mafunzo, 11 ni vyuo vikuu. 5 kampuni kupitia elimu ya mafunzo na ufundi na 13 ni kampuni za biashara.
Kauli mbiu ya maonesho hayo ni Elimu ya Ufundi na Mafunzo kwa Maendeleo ya Uchumi wa Viwanda Tanzania.
from MPEKUZI
Comments
Post a Comment