Korea Kaskazini: Tutaendelea kufanya majaribio ya makombora yetu na haturudi nyuma

Serikali ya Korea Kaskazini imesisitiza kwamba, itaendelea kufanya majaribio ya makombora yake na haitorudi nyuma katika suala hilo.

Taarifa iliyotolewa leo na Pyongyang imesema kuwa, kuacha kufanya majaribio ya makombora ya nchi hiyo, kuna maana ya kupuuza haki yake ya kujilinda. 

Kadhalika serikali ya Korea Kaskazini imeyataja kuwa yasiyo sahihi madai ya John Bolton, Mshauri wa Usalama wa Taifa wa Marekani kwamba majaribio hayo yanakiuka maazimio ya Umoja wa Mataifa. 

Ameongeza kwamba, majaribio ya makombora ya nchi hiyo ni jibu kwa vitisho na mashinikizo ya Washington na washirika wake katika eneo dhidi ya Pyongyang.

Imesema kuwa, imeamua kuanzisha majaribio ya silaha zake kutokana na kitendo cha Marekani cha kutofungamana na ahadi zake kwa ajili ya kuiondolea vikwazo Pyongyang na kadhalika hatua yake ya kufanya mazoezi ya kijeshi katika Rasi ya Korea kwa kushirikiana na waitifaki wake ambao ni Korea Kusini na Japan. 

Hivi karibuni pia serikali ya Korea Kaskazini ilitangaza kuwa Washington inapaswa kubadili siasa zake za upande mmoja kama sharti la kurejea kwenye meza ya mazungumzo kati yake na Marekani. 

Wizara ya Mambo ya Nje ya Korea Kaskazini ilisema kuwa Pyongyang haitarejea kwenye meza ya mazungumzo iwapo serikali ya Marekani haitafutilia mbali matakwa yake ya upande mmoja katika mchakato wa mazungumzo ya kudhibiti silaha za nyuklia.


from MPEKUZI

Comments