Bilioni 107.1 Zimetengwa Katika Utekelezaji Wa Ujenzi Wa Maabara Za Masomo Ya Sayansi Nchini.

Na.Faustine Gimu Galafoni,Dodoma.
Katika mwaka wa fedha 2019/2020 ,serikali imetenga  Jumla ya Tsh.Bilioni 107.1  katika  kutekeleza  mpango wa ujenzi wa maabara  za masomo ya sayansi kwa shule za sekondari   hapa nchini.
 
Hayo yamesemwa Mei 29,Bungeni jijini Dodoma na Naibu Waziri wa nchi,Ofisi ya Rais TAMISEMI Mhe.Mwita Waitara wakati akijibu swali la mbunge wa Mwanga Prof.Jumanne Maghembe  aliyehoji lini serikali itatenga fedha kwa ajili ya kukamilisha  maabara za sayansi  katika shule zote za kata hapa nchini.
 
Akijibu Swali hilo,Mhe.Waitara amesema serikali inatekeleza  mpango wa ujenzi  wa maabara za Masomo ya sayansi  katika shule za sekondari  kwa kushirikiana na wananchi na wadau  wa maendeleo wa ndani na nje  ambapo kwa mwaka wa fedha 2019/2020 ,serikali  imetenga Tsh. Bil.107.1   katika utekelezaji huo.

Kati ya Kiasi hicho,Tsh. Bilioni 58.2  kupitia mpango wa lipa  kulingana na matokeo [EP4R] na Tsh.Bilioni 48.9  kupitia mpango wa kuboresha  shule za sekondari [SEQUIP] ambapo sehemu ya Fedha hizo  zitatumika kukamilisha  ujenzi wa Maabara  za masomo ya sayansi  kwa shule za sekondari za kata nchini.
 
Hata hivyo,Naibu waziri Waitaraamesema serikali imejipanga namna ya kufanya vizuri katika Masomo ya Sayansi ambapo imeshatoa maelekezo namna ya ufundishaji kwa shule zenye changamoto ya vifaa vya maabara ili ufaulu kuongezeka mwaka hadi mwaka.


from MPEKUZI

Comments