Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika maadhimisho ya miaka 10 tangu kuanzishwa kwa Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote Nchini (UCSFA) yanayotarajiwa kufanyika leo hadi Aprili 30, mwaka huu.
Akizungumza jijini hapa jana, Mtendaji Mkuu wa UCSFA, Peter Ulanga, alisema Majaliwa anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika maadhimisho hayo yatakayokwenda sambamba na shughuli mbalimbali.
Alisema maadhimisho hayo yatakuwa pamoja na maonesho ya watoa huduma mbalimbali za mawasiliano nchini.
Ulanga alisema wamekusudia kutekeleza mradi wake wa kuunganisha shule na mtandao wa intaneti na kutoa vifaa vya tehama zikiwamo kompyuta, printa pamoja na projekta za kufundishia.
“Mradi huu utaenda sambamba na kutoa elimu ya mafunzo ya Tehama kwa walimu ili waweze kutatua changamoto mbalimbali zinazowakabili wakati wa utumiaji wa vifaa mbalimbali vya Tehama ili vifaa husika viweze kuleta tija katika shule husika,” alisema.
Pia alisema watatoa ruzuku ya ujenzi katika maeneo mbalimbali ya nchi hususan makao makuu ya wilaya ili kufikisha matangazo ya kidijitali ya runinga.
“Mfuko unachukua fursa hii kuualika umma wa wananchi wa Jiji la Dodoma kuhudhuria maonesho hayo. Sambamba na maonesho hayo mfuko utazindua Klabu za Tehama katika shule za sekondari Dodoma na Msalato,” alisema Ulanga.
Katika hatua nyingine, alisema tangu kuanzishwa kwake umetumia zaidi ya Sh bilioni 118 katika miradi mbalimbali katika kata 703 zenye vijiji 2,500 vyenye wananchi zaidi ya milioni tano.
“Tangu kuanzishwa kwa mfuko mwaka 2009 hadi sasa hivi 2019 umetumia shilingi bilioni 118 kufikisha mawasiliano katika kata 703 katika vijiji 2,500 vyenye watu zaidi ya milioni tano,” alisema.
from MPEKUZI
Comments
Post a Comment