Rais Magufuli Atoa Siku 7 Kwa Wakuu Wa Mikoa Inayozalisha Dhahabu Kufungua Masoko Ya Madini

Na Mwandishi Wetu,MAELEZO
RAIS Dkt. John Pombe Magufuli ametoa siku saba kwa Wakuu wa Mikoa inayozalisha dhahabu nchini kushirikiana na Wizara ya Madini katika kufungua masoko ya madini ikiwemo dhahabu ili kuifanya sekta ya madini kuweza kuleta tija ya kiuchumi kwa Watanzania wote hususani wachimbaji wadogo.

Akizungumza Mkoani Mbeya leo Jumamosi (April 27, 2019) wakati wa katika hafla ya uzinduzi na uwekaji wa jiwe la msingi la barabara ya Mbeya-Lwanjilo-Chunya-Makongosi yenye urefu wa Kilometa 111, Rais Magufuli alisema Serikali anayoiongoza kamwe haitokubali kuona wachimbaji wadogo wakiendelea kuteseka nchini.

Aliongeza kuwa tangu mwaka 2017, Serikali imepitisha Sheria Bungeni inayotoa maelekezo kuhusu usimamizi wa sekta ya madini nchini na hivyo anashangwa na baadhi ya Viongozi wake hususani Wakuu wa Mikoa inazozalisha dhahabu kusuasua katika kusimamia maelekezo ya maelekezo yake aliyoyatoa katika siku za nyuma.

Alisema kuwa Serikali pia imefuta kodi mbalimbali za madini na kuendelea kuwahamasisha wachimbaji wadogo kupeleka dhahabu zao katika masoko hayo, lakini hadi sasa baadhi ya Wakuu wa Mikoa wameshindwa kujenga masoko hayo, pamoja na faida mbalimbali zinazopatikana katika masoko hayo ikiwemo kuepusha dhuluma kwa wachimbaji, kupata dhahabu yenye ushindani pamoja na kuzuia upotevu wa kodi ya Serikali.

Aliongeza kuwa katika mkutano wake alioufanya hivi karibuni na Viongozi wa Wizara ya Madini na Wakuu wa Mikoa ya Tanzania Bara inayozalisha Dhababu, alitoa maelekezo ya kufungua masoko ya madini katika maeneo yao, ingawa ni Mkoa wa Geita pekee uliyotekeleza maelekezo hayo wakati ujenzi huo hauhitaji nyumba au eneo kubwa.

“Kama Mkoa wa Geita, umeweza kuwa na Kituo cha soko la kuuzia madini, nashangazwa kwanini Wakuu wengine wa Mikoa wanashindwa kutekeleza maelekezo hayo, hivyo hili ni agizo kwa Wakuu wa Mikoa ya Katavi, Singida na Arusha kuhakikisha kuwa watatekeleza maagizo haya” alisema Rais Magufuli.

Aidha Rais Magufuli alisema Serikali anayoiongoza haiwezi kuwa na Viongozi na Watendaji wasiotaka kutekeleza maagizo, hivyo ametoa kipindi cha muda huo kuhakikisha kuwa vituo hivyo vinafunguliwa na hivyo kuwahakikishia masoko ya uhakika wachimbaji wadogo ambao wamekuwa wakidhulumiwa dhahabu zao na baadhi ya wafanyabiashara wasio waaminifu.

Aidha Rais Magufuli aliutaka Uongozi wa Mkoa wa Mbeya hususani Wilaya ya Chunya kuhakikisha kuwa soko hilo la dhahabu linafunguliwa haraka iwezekanavyo kwa kuzingatia kuwa rasilimali zote muhimu za kufanikisha  maagizo hayo zipo ikiwemo vyombo vya ulinzi na usalama ambavyo vitatumika kwa ajili ya ulinzi wa madini ya dhahabu wakati wa mauzo hayo yakifanyika.

Kwa mujibu wa Rais Magufuli, alisema kuwa suala la kujiletea maendeleo kwa Watanzania linacheleweshwa na baadhi ya Viongozi Watendaji Serikali kwani wananchi hususani wachimbaji wadogo wa madini wamekuwa na juhudi kubwa za kujiletea maendeleo yao lakini wamekuwa wakikatishwa tamaa pamoja na juhudi kubwa wanazozionyesha katika kuchimba dhahabu.

Kwa upande wake, Waziri wa Madini, Dotto Biteko alisema tangu kutungwa kwa Sheria ya Madini mwaka 2017, Serikali imeweza kuokoa kiasi kikubwa cha madini kutoroshwa nje ya nchi, ambapo katika Wilaya ya Chunya ambayo ni Wilaya ya pili kwa uzalishaji wa dhahabu Serikali imeweza kutoa jumla ya kilo 30 zilizokuwa zikitoroshwa nje ya nchi kutokana na kukosekana kwa mtambo wa kuchenjulia madini.

Mara baada ya kujiridhisha na taratibu zote za kisheria, tumeweza kufungua mitambo 38 ya kuchenjulia dhahabu hapa Chunya, ambayo tulisimamisha shughuli hizi huko nyuma kutokana na utoroshaji mkubwa uliokuwa ukifanyika” alisema Biteko.


from MPEKUZI

Comments