Rais Magufuli Ataja Sababu za Kutengua Uteuzi wa Mkuu wa Wilaya ya Chunya

Rais John Magufuli amesema alimtoa aliyekuwa mkuu wa wilaya ya Chunya, Rehema Madusa kwa sababu alikuwa akichoma mazao ya wananchi kwa madai kuwa wamelima ndani ya hifadhi za wanyamapori.

Rais Magufuli ameyasema hayo jana Aprili 27, 2019  katika mkutano wa hadhara katika Viwanja vya Sabasaba wilaya ya Chunya mkoani Mbeya ikiwa ni mwendelezo wa ziara yake mkoani humo.

Alisema licha ya asilimia 32.5 ya eneo lote la Tanzania kuwa na wanyama lakini baadhi ya maeneo hayo yamechukuliwa na kiasi cha pesa kinachopatikana hakijulikani.

“Sasa kama fedha nyingine hatujui zinakokwenda inakuwaje mtu aliyeamua kulima katika eneo la hifadhi wewe umchomee, nilikuwa nimekaa naangalia katika televisheni mtu na rehema zake unamchomea chakula ili akale wapi,” alihoji Magufuli.

“Ukimchomea mahindi yake kesho tena utampelekea mahindi ya kula, kwa hiyo hata msitafute sababu nyingine ni hiyo,” amesema Magufuli

“Yalikuwa mambo ya ajabu sana, nikamuambia mkuu wa mkoa (aliyekuwa- Amos Makala) lakini nikaona na yeye anafanya mambo kidogo kidogo nikaona ngoja nimtoe Mbeya nimpeleke Katavi kwa uangalizi zaidi,”

“Ndiyo maana tukatengeneza timu ya mawaziri waangalie maeneo ambayo zamani yalikuwa hifadhi za wanyama na hayatumiki tutayakata yatakuwa maeneo ya watu.”


from MPEKUZI

Comments