Katibu Mkuu wa CCM, Dk Bashiru Ally amesema Mbunge wa Mtama, Nape Nnauye anahitaji kupikwa, kusikilizwa, kuaminiwa na kusimamiwa.
Dk Bashiri pia amemtaja Mbunge wa Nzega Mjini, Hussein Bashe akisema ni miongoni mwa vijana waliopitia katika Umoja wa Vijana wa CCM wakati mfumo wa kuandaa viongozi ukiwa umekufa.
Dk Bashiru alikuwa akizungumza katika mahojiano kupitia kituo cha televisheni cha ZBC2 kuhusu Muungano uliotimiza miaka 55.
Mhadhiri huyo wa zamani wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) alizungumzia pia umuhimu wa vijana kuandaliwa kupitia mifumo ya chama.
Julai 28, 2018, akizungumza na wanachama wa CCM mjini Nzega, Dk Bashiru alisema kuwa Nape na Bashe ni watukutu wanampa wakati mgumu kutokana na udadisi wao wa mambo mbalimbali wawapo bungeni, jambo linalowafanya Mawaziri wafikiri kwa kina kabla ya kutoa majibu na maamuzi.
“Nawafahamu wabunge hawa kuwa ni watukutu kwelikweli, wadadisi kwelikweli, lakini wanapishana, kwa kuwa Nape ni mdadisi na mtukutu ambaye joto lake ni kali, hivyo kazi yake ni kupoza,” alisema.
from MPEKUZI
Comments
Post a Comment