Waziri Mhagama Ahimiza vijana kuwa wazalendo kwa nchi yao

Na; OWM – KVAU, Kilimanjaro
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Mhe. Jenista Mhagama amewahimiza vijana kuwa wazalendo na kuithamini nchi yao.

Akizungumza wakati wa hafla ya kuwaaga vijana waliopanda Mlima Kilimanjaro jana tarehe 26 Machi, 2019 Mkoani Kilimanjaro ikiwa ni kuaadhimisha kumbukumbu ya miaka 20 ya kifo cha Baba wa Taifa Mwl. Julius Kambarage Nyerere.

Waziri Mhagama alisema kuwa, Baba wa Taifa Mwl. Julius K. Nyerere alikuwa kiongozi mzalendo kwa nchi yake na alijali utu na usawa, hivyo ni vyema vijana na vizazi vijavyo wakarithishwa falsafa za Baba wa Taifa.

“Vijana mna kila sababu kuyaenzi matendo ya Baba wa Taifa Mwl. Julius K. Nyerere na Mhasisi wa Mapinduzi ya Zanzibar, Abeid Amani Karume kwa vitendo kwa kuwa ninyi ndio nguzo ya Taifa na mnaelewa vema tulipotoka, tulipo na tunapoenda,” alisema Mhagama

Aliongeza kuwa, Viongozi hawa hawakuwa wabinafsi kwa kujilimbikizia mali na hawakubagua mtu kwa rangi wala kabila bali walijenga Taifa na kudumisha amani na moja.

Aliendele kwa kuwapongeza vijana kwa azma yao ya kuenzi historia na mazuri yaliyofanywa na viongozi hao kwa kupanda mlima Kilimanjaro na kuwatakia baraka waende na kurudi salama.

“Kitendo hiki ni cha kishujaa na uzalendo wa hali ya juu kwa Taifa ikiwa ishara ya kumuenzi Baba wa Taifa,” alieleza Mhagama

Aidha Waziri Mhagama alitoa rai kwa vijana kuwa wazalendo na kuwasihi wafanye kazi kwa bidii ili kujenga Taifa kupitia uchumi wa viwanda utakao ifikisha Tanzania kwenye uchumi wa kati ifikapo mwaka 2025.

Alifafanua kuwa uzalendo lazima ujengwe sambamba na ujenzi wa uchumi wa Taifa, ulinzi na usalama wa Taifa na utunzaji wa tunu za Taifa.

Pamoja na hayo, aliwapongeza na kuwashukuru Viongozi wa Mkoa wa Songwe na Lindi pamoja na uongozi wa Hifadhi ya Mlima Kilimanjaro (KINAPA) kwa ushirikiano mkubwa na Ofisi yake katika kuwashirikisha vijana kwenye suala hilo.

Kwa Upande wake Mkuu wa Wilaya ya Moshi, Mhe. Kippi Warioba alisema kuwa tukio hili ni muhimu kwa vijana kutambua historia na mchango wa Baba wa Taifa Mwl. Julius Nyerere katika Taifa.

“Tumieni fursa hii kupitia vitabu mbalimbali vya kihistoria ili mjifunze mipango, mwenendo na malengo ya Baba wa Taifa itawasaidia na kuwajengea nafasi nzuri ya kujitambua na kuelewa historia ya Taifa,” alisema Warioba.

Naye Mkurugenzi wa Maendeleo ya Vijana, Bw. James Kajugusi alieleza kuwa Baba wa Taifa alianza harakati za kulikomboa Taifa akiwa kijana na aliendelea kufanya hivyo kwa kuwa hamasisha vijana kujenga Taifa lao baada ya kupata uhuru.

MWISHO


from MPEKUZI

Comments