Mdhamini wa Tundu Lissu Aomba Kujitoa.....Mahakama Yagoma

Mdhamini wa Mbunge Tundu Lissu, Robert Katula, katika kesi ya uchochezi inayomkabili Lisu na Wahariri wa gazeti la Mawio, amemuomba Hakimu Thomas Simba kujitoa kuwa mdhamini wa Lissu, kwa kile alichokidai amekosa ushirikiano kwa mshtakiwa huku Mahakama ikikataa ombi lake.

Katula ametoa madai hayo leo Jumatatu Machi 25, katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba, baada ya mahakama kutaka maelezo yake kuhusu mshtakiwa Lissu.

“Mheshimiwa sina la kusema, sina taarifa naye, hana ushirikiano kwa kweli, ikiwezekana nijitoe,”alidai. 


Wakili wa Serikali, Patrick Mwita amedai kuwa maneno aliyosema mdhamini kuwa mshtakiwa hajui alipo na jukumu lake ni kuhakikisha mshtakiwa anafika mahakamani si sahihi hivyo kuomba kumpeleka mshtakiwa.

Mdhamini wa pili Ibrahim Ahmed alidai kuwa wametafuta kila namna ya kupata mawasiliano ya Lissu anakotibiwa hawakufanikiwa kumpata lakini kwa kuwa jukumu lake ni kufika mahakamani ameona ni vyema kufika na kutoa taarifa.

Baada ya maelezo hayo, Hakimu Simba alieleza kuwa wamekuwa wakitegemea kupata maendeleo kutoka kwa wadhamini kwa ajili ya kuweka rekodi hivyo hakuna mdhamini atakayeweza kujitoa mshtakiwa akiwa hayupo mahakamani.

Kesi hiyo imeahirishwa hadi Aprili 25, 2019 kwa ajili ya kutajwa na washtakiwa wote wako nje kwa dhamana.


from MPEKUZI

Comments