Lugola Atangaza Vita Dhidi Ya Matrafiki Wala Rushwa Akifungua Kongamano La Taifa La Usalama Barabarani

Na Felix Mwagara, MOHA.
WAZIRI wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Kangi Lugola amewataka Askari Polisi Kikosi cha Usalama barabarani nchini, kusimamia sheria kikamilifu na kujiepusha na vitendo vya rushwa ili kuokoa maisha ya watu wasio na hatia ambao hufariki, kupata ulemavu wa kudumu kutokana na ajali.

Akizungumza kabla ya kulizindua kongamano la kitaifa la wadau wa usalama barabarani nchini, Lugola ambaye pia alikuwa mgeni rasmi katika kongamano hilo, alisema wasimamizi wa Sheria wakisimamia sheria kikamilifu na elimu ikaendelea kutolewa kwa watumiaji wengine wa barabarani na wakabadili tabia zao, uwezekano wa kupunguza ajali zaidi ni mkubwa.

“Usalama Barabarani unaanza na kila mmoja wetu, nawaomba sana tutumie fursa hii kikamilifu kwa kutoa mawazo na maoni yetu katika kongamano hili kwa manufaa na mustakabali wa Usalama wetu hivi sasa na vizazi vijavyo,” alisema Lugola.

Pia aliwataka wadau hao, watumie fursa ya kongamano hilo kuzungumza kwa uwazi, kutoa mawazo yao ambayo yanalenga kuboresha utendaji wa Baraza Usalama Barabarani na vyombo vingine ambavyo vinasimamia Sheria ya Usalama Barabarani.

Lugola alisema Lengo la Serikali ya Awamu ya Tano chini ya Rais Dkt. John Pombe Joseph Magufuli ni kutokomeza ajali za barabarani nchini, hivyo aliwataka wadau wa usalama barabarani wajipange kikamilifu kwa kiuweka mikakati thabiti kwa lengo la kutokomeza ajalin nchini.

“Ni wazi kwamba wasimamizi wa Sheria wakisimamia sheria kikamilifu na elimu ikaendelea kutolewa kwa watumiaji wengine wa barabarani na wakabadili tabia zao, uwezekano wa kupunguza ajali zaidi ni mkubwa,” alisema Lugola.

Pia Waziri Lugola alilitaka Baraza la Usalama barabarani kusimamia utekelezaji wa Mpango Mkakati wa Baraza Awamu ya Nne, ambao umezinduliwa Waziri huyo ameuzindua na Muongozo wa Utendaji na Utekelezaji wa majukumu ya Kamati za Usalama Barabarani za Mikoa na Wilaya ili kudhibiti ajali za Barabarani na Kuimarisha Utendaji wa Kamati.

Lugola pia aliwataka kusimamia ukaguzi wa magari ili Kuhakikisha Magari mabovu yanaondoka barabarani, na Baraza likamilishe Uundwaji wa Kamati za Usalama Barabarani za Mikoa na Wilaya haraka ili Kamati hizo zianze kazi ili kwenda na Mabadiliko yanayofanyika ndani ya Baraza.

Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, ambaye pia ni Mwenyekiti wa Baraza Taifa la Usalama Barabarani, Mhandisi Hamad Masuani alisema takwimu za usalama barabarani zimepungua nchini kutokana na Baraza lake kuweka mikakati za kupambana na ajali nchini.

Kongamano hilo ni mbadala wa Wiki ya Nenda kwa usalama barabarani ambayo kila mwaka ufanyika katika mkoa ambao uchaguliwa na wajumbe wa Baraza hilo.


from MPEKUZI

Comments