Aliyekuwa dereva wa Rais wa zamani wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) Jamal Malinzi, Steven John, ameileza mahakama alikuwa anachukua fedha kutoka kwa aliyekuwa mhasibu wa shirikisho hilo, Hellen Ndaro na kumpelekea Malinzi.
Aidha, dereva huyo ambaye ni shahidi katika kesi hiyo ya utakatishaji fedha inayomkabili Malinzi na wenzake, baada ya kujitambulisha alishindwa kuongea akawa anatiririka machozi.
Hakimu Mkazi, Maira Kasonde wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, alimuita shahidi huyo lakini alinyamaza kimya huku akifuta machozi.
“Macho yameaanza kuuma au una tatizo gani shahidi? alihoji hakimu wakati shahidi anafuta machozi.
Dereva huyo amedai hajawahi kumchukulia fedha Malinzi mara mbili kwa siku moja na kwamba wakati anachukua fedha hizo alikuwa akisaini fedha lakini wakati akimkabidhi Malinzi hakuwa anasaini.
Shahidi huyo akiongozwa na Wakili wa Serikali kutoka Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Leonard Swai, amedai Septemba 26 mwaka 2016, alimpelekea Malinzi Dola za Marekani 28,650 na Dola 24,000.
Septemba 26 mwaka 2016 alimpelekea Sh milioni nne na kwamba yeye ndiyo alikuwa akisaini hati za malipo kwa niaba ya Malinzi.
Washtakiwa wengine katika kesi hiyo ni Mhasibu wa TFF, Nsiande Mwanga, Meneja wa Ofisi TFF, Miriam Zayumba na Karani wa TFF, Flora Rauya ambao kwa pamoja wanakabiliwa na mashitaka 30 yakiwamo ya kula njama, kughushi, kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu na utakatishaji wa dola za Marekani 173,335.
Malinzi, Mwesigwa na Nsiande wanaendelea kusota rumande kwa sababu wanakabiliwa na mashitaka ya utakatishaji fedha ambayo hayana dhamana kwa mujibu wa sheria.
from MPEKUZI
Comments
Post a Comment