Kifo cha Mkurugenzi wa Vipindi wa Clouds Media Group, Ruge Mutahaba kimewashtua wengi, miongoni ni wanasiasa ambao wametumia mitandao yao ya kijamii kuelezea hisia zao na kutoa salamu za pole.
Miongoni mwa wanasiasa waliomzungumzia Ruge ni Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, January Makamba ameandika kwenye Twitter akisema, “Ruge. Ruge. Ruge. Nakosa maneno ya kutosheleza kuelezea maumivu na huzuni niliyonayo.”
“Kwa sasa, dua na fikra zangu ni kwa mama, Dk Mutahaba, ndugu na marafiki ambao walihangaika sana kuhakikisha anapona. Nikipata nguvu nitasema zaidi. Tangulia jamaa yangu, tunakuja. #RIPRuge.”
Mbunge wa Mbeya Mjini (Chadema), Joseph Mbilinyi ‘Sugu’ ameandika kwenye Instagram, “Sikutaka kuamini habari hii mpaka nimezungumza na Joseph Kusaga na kaniambia ni kweli umetutoka!”
“Pole sana kwa familia, Clouds Media Group, uongozi na wafanyakazi wote pamoja na wadau wote wa tasnia ya muziki na burudani tulioguswa na msiba huu mzito... R.I.P RUGE.”
Waziri wa zamani wa mambo ya ndani, Mwigulu Nchemba ameandika, “Umeondoka Ruge Mutahaba, umeondoka shujaa, umeondoka mpambanaji.”
“Pole kwa familia, ndugu na jamaa, pole zaidi kwa Watanzania wote kwa msiba huu mzito.”
“Najua ya kuwa waweza kufanya mambo yote na ya kuwa makusudi yako hayawezi kuzuilika" Ayubu 42:2,” ameandika Mwingulu kwenye akaunti yake ya Instagram akiambatanisha na picha ya Ruge.
Mbunge wa Mtama (CCM), Nape Nnauye ameandika kwenye Twitter akisema, “Pumzika kwa amani kaka! Huna mfano wako duniani, maisha yako yameacha alama kubwa, utaishi milele kwa wema wako! Ndugu, Rafiki na mzalendo wa kweli!”
from MPEKUZI
Comments
Post a Comment