Na Stella Kalinga, Simiyu
Naibu waziri Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia watu wenye ulemavu, Mhe. Stella Ikupa amewashauri Vijana nchini, kuondokana na dhana ya kuwa shughuli za kilimo ni za Wazee na badala yake watumie vitalu nyumba kujifunza kilimo chenye tija na hatimaye waweze kujikwamua kiuchumi.
Ikupa ametoa ushauri huo wilayani Maswa wakati alipowatembelea Vijana katika kitalu nyumba katika kata ya Binza akiwa katika ziara yake wilayani humo Mkoani Simiyu Februari 25, 2019.
IKUPA amesema Vijana wanapaswa kuachana na dhana potofu kuwa kilimo ni shughuli inayopaswa kufanywa na Wazee, badala yake watumie fursa za mafunzo ya kilimo na wakawe mabalozi ndani ya jamii kuwa kilimo kinaweza kuwapatia ajira na kipato.
“ Kilimo kinaweza kuwatoa vijana kutoka mahali fulani kikawapeleka mahali pengine tena wakawa na uwezo mzuri kifedha kuliko hata wale walioajiriwa katika kazi za maofisini, niwashauri vijana muione fursa kupitia vitalu nyumba ondoeni dhana kwamba eti kilimo ni kazi ya wazee si kweli” alisema.
Ameongeza kuwa vijana wanayo nafasi ya kupata mikopo kupitia Mfuko wa Maendeleo ya Vijana kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu na Halmashauri zao hivyo wachangamkie fursa hiyo kupata mikopo itakayowawezesha kuendeleza shughuli zao za uzalishaji ikiwemo kilimo kupitia vitalu nyumba.
Katika hatua nyingine Mhe. Ikupa amesema ni vema Halmashauri zikazingatia masuala ya watu wenye ulemavu katika mipango ya bajeti zao ili ziweze kusaidia katika utatuzi wa baadhi ya changamoto za watu wenye ulemavu.
Aidha, amesisitiza umuhimu wa kuwatumia wakalimani wa lugha ya alama ili waweze kusaidia mawasiliano kati ya walemavu wa kusikia na makundi mbalimbali ya watu ikiwemo viongozi.
Naye Mkuu wa Wilaya ya Maswa, Mhe. Dkt. Seif Shekalaghe amekiri kupokea maelekezo yote yaliyotolewa na Mhe. Naibu Waziri Ikupa na kumhakikishia kuwa watu wenye ulemavu watalindwa, watashirikishwa katika fursa mbalimbali ikiwa ni pamoja na mradi wa Kitalu nyumba.
Nao baadhi ya vijana wanaojihusisha na utekelzaji wa mradi wa Kitalu nyumba katika Kata ya Sola wameishukuru Serikali na kuomba ipanue wigo wa kuwafikia vijana kupitia mradi huu ili vijana wengi waweze kufikiwa mpaka ngazi ya Kata.
“ Mimi ninaishukuru Serikali yetu kwa kutuletea mradi wa kitalu nyumba, tumeshajifunza namna ya kutengeneza vitalu nyumba, kilimo bora chenye tija kupitia mradi huu, tunaomba mradi upelekwe mpaka ngazi ya kata ili vijana wengi waweze kunufaika zaidi” alisema Rachel Paulo mkazi wa Sola Maswa.
Naibu Waziri Ikupa, anaendelea na ziara yake Mkoani Simiyu ambayo itahitimishwa tarehe 27 Februari 2019, akiwa wilayani Maswa Naibu waziri ametembelea kitalu nyumba kilichopo Sola na kuzungumza na viongozi wa Serikali na watu wenye ulemavu.
from MPEKUZI
Comments
Post a Comment