Makamu wa Rais Mama Samia Suluhu

Makamu wa rais Samia Suluhu amefanya mazungumzo na wadau mbalimbali wa mazingira Mkoani Tabora, ambapo amewataka kuboresha usafi na kuacha kukata miti kutokana na matumizi ya mkaa na kuni kuchangia uharibifu wa mazingira mkoani humo kwa kiasi kikubwa.

Ameyasema hayo leo Februari 25, mwaka huu katika kongamano la kujadili mustakabali wa mazingira mkoani humo ambapo amewataka wazazi kuwafundisha watoto na vijana juu ya utunzaji wa mazingira ili waweze kusaidia kupambana na uharibifu huo.

“Fursa mliyo nayo ni wingi wa watu hapa nimeona kuna vijana na watoto wengi sana na wanakuwa hivyo tusipowafundisha jinsi ya kutunza na kuhifadhi mazingira tutaiweka nchi yetu katika hali ambayo sio nzuri, tuangalie ni kazi gani tunawapangia ili wanavyozidi kukua waweze kujua wanatunza vipi mazingira yao,” amesema.

Aidha amesema kuwa mazao yanayolimwa mkoani humo ni ya uchumi wa viwanda na uchumi huo unahitaji umeme ili viwanda viweze kufanya kazi vizuri hivyo amesisitiza utunzaji wa mazingira ili bwawa liweze kujazwa na kuwe na umeme wa kutosha.

“Makundi ya ng’ombe yakikanyaga ardhi wanaharibu mfuko wa ikolojia na kinyesi cha wanyama kinafanya ardhi inakuwa ngumu na kupasuka hivyo jaribuni kutumia utajiri huo mlio nao vizuri kwaajili ya kuleta maendeleo,” amesema.


from MPEKUZI

Comments