Na Amiri kilagalila
Shirika la umeme Tanzania (TANESCO) mkoa wa Njombe limewataka Mafundi wanaojihusisha na shughuli za nishati ya umeme mkoa wa Njombe kupata leseni kutoka mamlaka ya udhibiti wa nishati na maji EWURA ili kupambana na vishoka wanaosababisha matatizo kwa wateja.
Wito huo umetolewa na YUSUPH SALIM mhandisi wa mpango na kaimu meneja wa Tanesco mkoa wa Njombe wakati akizungumza na mafundi umeme pamoja na wahandisi mkoa wa Njombe katika mkutano wa pamoja ulioandaliwa na umoja wa makandarasi (UMAU) katika ukumbi wa Miriam hotel mjini Njombe ukiwa na lengo la kufahamiana na kubaini changamoto ya kazi zao.
“Fundi yeyote kwa sasa mkoani Njombe anatakiwa awe na leseni ya Ewura na hii kupata ni mda mfupi sana tena kwa gharama ndogo ya elfu 60 tu, sidhani kama kuna fundi atashindwa hili,kigezo cha kwanza mtu anapokwenda kufanya kazi katika nyumba yeyote awe na leseni, wateja wetu niwaombe tusifanye kazi na watu wasiokuwa na vigezo ili hata ikitokea matatizo aweze kushtakiwa na kunyang’anywa leseni pamoja na kuchukuliwa hatua nyingine”alisema SALIM mhandisi wa Mpango
Aidha amewataka wakandarasi mkoani humo kuacha tabia ya kwenda kwa wateja na kufanya kazi kama tanesco kwa kuwaongopea wananchi hususani vijijini wakidai kuwapelekea nishati ya umeme wakati jukumu hilo lipo chini ya shirika la umeme nchini Tanesco.
Baadhi ya makandarasi akiwemo KANDIDUS PATA pamoja na Eng.GODY NUNGWI wamesema mafundi wamekuwa wengi mitaani kutokana na vyuo kuzalisha wataalamu wa kutosha lakini wanaanza kufanya kazi bila leseni huku wakiwanyonya wakandarasi kwa mapatano ya bei yoyote na mteja kwani hawana kodi yeyote ya serikali.
“Tunataka hawa mafundi wajitahidi wawe na leseni ya EWURA ukiangalia hawa mafundi kwa mkoa wa Njombe wako wengi na wakandarasi hatuzidi kumi na nne ina maana huku mitaani ni kama wanaibia serikali halafu sisi wakandarasi ambao tunalipa mapato, tunalipia leseni wanatuhujumu”alisema mmoja wa makandarasi
ZAKARI MWACHISE na ORESTA MGAYA ni baadhi ya mafundi umeme walioshiriki mkutano huo wamekubali kuwepo kwa changamoto baina yao na makandarasi pamoja na uwepo wa vishoka wanaofanya kazi bila ukamilifu huku wakiridhia makubaliano yaliyotolewa katika kikao hicho ikiwemo umiliki wa leseni.
Kwa upande wake EDGA BOSCO MTITU ambaye ni katibu wa umoja wa makandarasi na mafundi umeme UMAU mkoa wa Njombe amesema kuna vitu havikuwa sawa baina makandarasi,mafundi na tanesco ikiwemo tanesco kuingilia kazi za makandarasi hivyo wanaimani kupitia mkutano huo wamewekana sawa na kusisitiza agizo la Tanesco kwa mafundi kuwa na leseni ya Ewura.
“Awali hatukuwa na umoja lakini kwa sasa tuna umoja wetu na moja ya lengo letu kuu kwanza ni kudhibiti vishoka na kila mmoja afanye kazi kulingana na nafasi yake na kwa sasa umoja huu tutaweza kutambuana kila mtu anayefanya kazi ya umeme kwa kuwa baadhi ya wateja wamekuwa wakilalamika kufanyiwa kazi mbovu na watu hawatambuliki na kwa sasa tunaimani kazi yeyote ikihalibiwa tutakuwa na uwezo wa kumtafuta aliyefanya kazi hiyo”alisema Mtitu katibu wa umoja wa mafundi.
from MPEKUZI
Comments
Post a Comment