CUF Upande wa Maalim Seif Waiangukia Mahakama

Chama cha Wananchi (CUF) kimeiomba Mahakama kutoa hukumu ya shauri lao namba 23/2016 linalohusu uhalali wa uenyekiti wa Profesa Ibrahim Lipumba kwa chama hicho.

Chama hicho upande wa Katibu Mkuu, Maalim Seif Sharif Hamad kimesema ucheleweshwaji wa hukumu ya  shauri hilo unawasababishia madhara ikiwamo kuibiwa fedha za ruzuku zaidi ya Sh1.5 bilioni, kuondolewa kwenye nafasi za uongozi na kuwapo kwa mashauri mengi mahakamani yanayowagharimu fedha na muda.

Hayo yamesemwa leo Jumanne Februari 26, 2019 na wabunge wake, Ally Saleh (Malindi) na Hamidu Bobali wa Mchinga wakati wakizungumza na waandishi wa habari katika ofisi za wabunge wa chama hicho, Magomeni jijini Dar es Salaam.

Saleh ambaye ni mnadhimu wa kambi ya CUF bungeni amesema si lengo lao kutoa shinikizo la aina yoyote, kuingilia taratibu za mahakama ila wanaomba shauri hilo litolewe hukumu.

"Tupo tayari kwa hukumu yoyote itakayotolewa, ila tumepata mashaka namna shauri hilo linavyoahirishwa mara kwa mara licha ya kuwa limeshasikilizwa," amesema Saleh.

"Kwa heshima na taadhima tunamuomba Jaji Mkuu na Jaji Kiongozi waliangalie suala hili kwa umuhimu na uzito maalumu kwa sababu kuchelewa kwake kunakiathiri chama chetu kwa kiasi kikubwa," amesema.

Amefafanua baadhi ya athari wanazopata tangu kupandikizwa kwa mgogoro huo ni kupoteza wabunge, madiwani na wenyeviti wa mitaa hata kwenye maeneo ambayo kichama wapo vizuri.

Ameitaja athari nyingine ni kuwapo kwa mashauri kadhaa Mahakama Kuu yanayowagharimu rasilimali fedha na muda na kuibiwa ruzuku zaidi ya Sh1.5 bilioni na uharibifu wa mali za chama zikiwamo magari na majengo.

"Chama kinashindwa kuendesha shughuli kwa utulivu na kujiandaa na chaguzi za ndani na za kiserikali kwa mwaka huu 2019 na uchaguzi mkuu 2020" amesema Saleh.

Naye Bobali amesema athari anazopata ni kubwa ikiwamo kutofanya siasa kwa kipindi chote tangu mgogoro huo ulipoanza.

Bobali ambaye pia ni mwenyekiti wa vijana wa chama hicho amesema mgogoro huo unawatoa kwenye ushindani wa kisiasa kwa sababu unawaweka mbali na wanachama wao na majimbo yao kwa ujumla.

"Tunashindwa kufanya siasa, kwa sababu baadhi ya maeneo wenyeviti wa chama kwa eneo husika wanakuwa upande wa Lipumba na sisi tupo upande halali wa Maalim Seif, huu mkanganyiko unatusukuma kuiomba mahakama kutoa hukumu ya kesi hiyo ili tuendelee na majukumu yetu angalau kwa kipindi hiki kifupi kabla ya uchaguzi mkuu 2020," amelalama Bobali.

Februari 22, 2019 Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam ilisogeza mbele utoaji  hukumu ya mgogoro wa uongozi ndani ya CUF na sasa hukumu hiyo itatolewa Machi 17, 2019.


from MPEKUZI

Comments