Ufaransa Yazitaka nchi za Umoja Wa Ulaya kuisusia Uingereza

Rais Emmanuel Macron wa Ufaransa amezitaka nchi wanachama wa Umoja wa Ulaya (EU) kususa kufanya mazungumzo mapya na Uingereza kuhusu makubaliano ya kujiondoa kutoka umoja huo, maarufu kama Brexit.

Alisema licha ya hayo zinapaswa kujiandaa kwa uwezekano wa kutokea hali ngumu baada ya Uingereza kujitoa kutoka Umoja wa Ulaya Machi mwaka huu.

Akizungumza kwenye mkutano wa tano wa kilele wa Ulaya Kusini uliofanyika Nicosia nchini Cyprus, aliitaka Uingereza ijikite katika makubaliano ya awali ili kuepuka kujitoa EU bila makubaliano.

Taarifa iliyotolewa na mkutano wa kilele wa Ulaya Kusini imesema, Umoja wa Ulaya utajitahidi kuifanya Uingereza ijitoe kwenye Umoja huo kwa utaratibu.

Lengo la kufanya hilo ilisema ni kuhakikisha uthibitisho wa raia na kampuni pamoja na kuharakisha maandalizi ili kukabiliana na changamoto zitakazotokana na ondoko la Uingereza umojani humo.

Kauli hiyo inakuja baada ya Waziri Mkuu wa Uingereza Theresa May kujipanga kurudi kwenye umoja huo katika jitihada za kujadili tena vipengele muhimu vya mpango wake kuhusu mchakato wa Brexit.

Uamuzi wa May unakuja baada ya wabunge wa Uingereza kupiga kura juu ya mapendekezo saba yaliyochaguliwa na Spika wa Bunge yaliyolenga kuleta mabadiliko katika mchakato wa awali wa Brexit.

Wabunge hao walipitisha mabadiliko yanayoitaka serikali kuepusha uwezekano wa Uingereza kuondoka Umoja wa Ulaya bila ya mkataba ifikapo Machi 29.

Lakini ishara zote zinaonyesha May atakuwa katika malumbano mapya na EU baada ya kuahidi kubadili makubaliano yaliyofikiwa awali kuhusu mchakato huo.

Mpango huo alioufanikisha baada ya mwaka mmoja na nusu wa majadiliano na EU, hata hivyo ulikataliwa na wabunge wa Uingereza, waliotaka mabadiliko katika vipengele fulani.

Katika kujaribu kuyafufua mazungumzo ya Brexit yaliyokwama, May amepewa jukumu na Bunge la nchi yake la kurudi kwenye makao makuu ya Umoja wa Ulaya ili kuzungumzia tena makubaliano aliyoafikiana na EU.

May anapanga kujadili na EU juu ya kipengele kinachohusu suala lenye utata la mpaka wa Ireland kilichokwisha kutiwa saini na nchi 27 wanachama wa Umoja wa Ulaya ambacho sasa Uingereza inataka kibadilishwe.

Hata hivyo, viongozi wa nchi za Umoja wa Ulaya wamesisitiza kuwa kipengele hicho hakiwezi kubadilishwa.

Msemaji wa Rais wa Baraza la Umoja wa Ulaya, Donald Tusk amesema suala hilo la mpaka wa Ireland ni sehemu ya mkataba juu ya Uingereza kujiondoa EU na kwamba haliwezi kujadiliwa upya.

Binafsi May anatambua kuwa Umoja wa Ulaya hauna hamu wala hautaki kuubadilisha mpango wa Brexit uliopo sasa, lakini ameahidi kwenda mjini Brussels na kutafuta mabadiliko makubwa na ya kisheria kuhusu mkataba huo.


from MPEKUZI

Comments