Marekani imesema kuna mashaka kuwa Korea Kaskazini haikutekeleza ahadi yake ya kuharibu vinu vya silaha za kinyuklia na kuachana na mpango huo licha ya kusaini makubaliano kati ya nchi hizo mbili.
Rais wa Marekani, Donald Trump na Rais wa Korea Kaskazini, Kim Jong-un walisaini makubaliano yaliyopunguza taharuki ya kiusalama kati ya nchi hizo mbili walipokutana Juni mwaka jana nchini Singapole.
Mkurugenzi wa Intelijensia wa Taifa, Dan Coats aliyeambatana na maafisa wengine waandamizi jana aliliambia Bunge la Senate uchunguzi wao unaonesha kuwa Korea Kaskazini haina mpango wa kuharibu kabisa silaha za nyuklia.
Korea Kaskazini imekuwa ikiweka sharti la kuwa Marekani inapaswa kuondoa vitisho vyote vya mashambulizi ya kinyuklia dhidi yake ndipo iharibu silaha zote za nyuklia.
Aidha, Coats ameiambia Senate kuwa kuna hatari ya China na Urusi kuandaa mashambulizi ya kimtandao (cyber attack) dhidi ya Marekani, akihofia kuwa inalenga kuingilia uchaguzi mkuu ujao.
CNN imeripoti kuwa utafiti uliofanywa na Idara ya Intelijensia ya Marekani umeonesha kuna hatari kubwa zaidi kuwahi kutokea tangu miaka ya 1950, kwa China na Urusi kufanya mashambulizi ya kimtandao dhidi ya nchi hiyo.
Marekani imekuwa ikiitupia lawama Urusi kuwa iliingilia uchaguzi uliompa ushindi Rais Donald Trump dhidi ya Hillary Clinton, madai ambayo Urusi imeyakanusha vikali.
from MPEKUZI
Comments
Post a Comment