Zao la Korosho katika kipindi kilichoishia Januari 2018 liliingizia Taifa fedha za kigeni shilingi 1,136,609,586,722 ikilinganishwa na mazo mengine ya biashara.
Akijibu swali la Mbunge wa Mtwara Mjini, Mhe. Maftaha Abdallah Nachuma, Naibu Waziri wa Kilimo, Mhe. Omari Mgumba, amesema licha mchango huo katika uchumi wa Taifa, zao la korosho limekuwa likikabiliwa na changamoto mbalimbali ambazo Serikali imekuwa ikizitafutia ufumbuzi ikiwemo kuongeza bei ya korosho na kutafuta masoko ya uhakika.
Mhe. Mgumba amezitaja changamoto hizo kuwa ni kuyumba kwa bei ya korosho katika soko la dunia kutokana na zao hilo kuuzwa likiwa ghafi yaani bila kuongezwa thamani, tija ndogo katika uzalishaji, baadhi ya wakulima kutotumia miche bora na matumizi hafifu ya pembejeo ikiwemo viuadudu kama salfa na wakulima kutozingatia kanuni bora za kilimo katika uzalishaji.
Aidha, Mhe. Mgumba amezitaja changamoto nyingine kuwa uvunaji na uhifadhi hafifu wa korosho, uwezo mdogo wa maghala ya kuhifadhia korosho na baadhi ya wakulima kuchanganya zao hilo na mawe na mchanga kwa ajili ya kuongeza uzito wakati wa mavuno.
“Katika kukabiliana na changamoto hizo, Serikali imeboresha mfumo wa uuzaji wa korosho kwa kuimarisha usimamaizi na ukaguzi kuanzia ngazi ya vyama vya msingi, maghala makuu, maghala aya hifadhi na kutoa elimu, kurejesha kwa kiwanda cha BUCCO cha mkoani Lindi cha ubanguaji wa korosho, ujenzi wa maghala matatu ya kuhifadhia korosho katika mikoa ya Lindi, Pwani na Tanga ili kuongeza kiwango cha uhifadhi na ubora wa korosho pamoja na kuzalisha miche bora 10,000,000 na kuisambaza kwa wakulima bure,”alisema Mgumba.
Naibu Waziri Mgumba ameongeza kuwa mikakati mingine ni pamoja na kuimarisha mnyororo wa thamani katika zao la korosho ili kuongeza uzalishaji, kuimarisha usambazaji wa pembejeo za kilimo kwa wakati, kutoa huduma za ugani pamoja na kuweka mazingira wezeshi na kuwajengea uwezo wabanguaji wa ndani kwa lengo la kuongeza thamani ya korosho inayozalishwa nchini.
Akijibu swali la nyongeza kutoka kwa Mbunge wa Mtama, Mhe. Nape Nnauye aliyetaka kujua hatua zilichukuliwa na Serikali kuhusu vitendo vya rushwa katika kuhakiki ununuzi wa Korosho, Waziri wa Kilimo, Mhe. Japhet Hasunga alisema kuwa wote waliojihusisha na vitendo hivyo hatua kali zilichukuliwa dhidi yao ikiwemo kusimamishwa kazi.
Serikali ya Awamu ya Tano imekuwa na dhamira ya dhati ya kuwainua wakulima nchini ikiwemo wa korosho kwa kuongeza bei ya korosho na kusimamia ununuzi wake. Jambo ambalo limekuwa kichocheo kwa wakulima wengi katika mikoa ya Lindi, Mtwara, Pwani na Tanga kujikita katika kilimo hicho.
Mhe. Rais Dkt. John Pombe Magufuli mwishoni mwaka 2018 alisema Serikali itanunua korosho kwa bei ya shilingi 3,300 kwa kilo. Jambo ambalo lilifanyiwa kazi na wakulima wa zao hilo wanafurahia bei hiyo na kutambua kuwa Serikali inawajali.
from MPEKUZI
Comments
Post a Comment