Kilichoendelea Leo Mahakamani Katika Kesi ya Zitto Kabwe na Spika Ndugai

Kesi ya Zitto Vs. Spika Ndugai kuomba tafsiri ya Mahakama kuhusu madaraka ya Bunge kumuita na kumuhoji CAG (Miscellaneous Civil Cause No. 1/2019) imeahirishwa hadi Februari 15 itapoitwa tena kwa ajili ya kusikilizwa

Kesi hiyo ya Kikatiba  imefunguliwa Mahakama Kuu na mbunge wa Kigoma Mjini (ACT-Wazalendo), Zitto Kabwe dhidi ya Spika wa Bunge, Job Ndugai na Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG).

Katika kesi hiyo, Zitto ambaye pia ni Kiongozi wa ACT anaiomba Mahakama Kuu itoe tafsiri ya  kinga ya CAG, Profesa Mussa Assad  iliyopo kikatiba na pia kutoa tafsiri ya Sheria ya Haki, Kinga na Madaraka ya Bunge katika kushtaki watu wanaosemekana kulidharau Bunge.

Kesi hiyo inayosikilizwa na jopo la majaji watatu; Firmin Matogolo (kiongozi wa jopo),  Dk Benhajj Masoud na  Elinaza Luvanda  imetajwa leo Alhamisi Januari 31, 2019 kwa mara ya kwanza mahakamani hapo na mahakama hiyo ikapanga kuanza kuisikiliza rasmi Februari 15, 2019.

Pia,  mahakama hiyo leo imewaamuru wadaiwa (Spika na AG) kuwasilisha mahakamani hapo utetezi wao ndani ya siku 14, ambazo zinaishia Februari 13, 2019.

Wakati kesi hiyo ilipotajwa leo, Zitto hakuwepo mahakamani na aliwakilishwa na wakili wake,  Fatma Karume huku Ndugai akiwakilishwa na jopo la mawakili watatu wa Serikali, wakiongozwa na mwanasheria wa Serikali Mkuu (PSA), Alesia Mbuya.

Zitto alifungua kesi hiyo baada ya Ndugai kupitia kwenye vyombo vya habari na baadaye kumwandikia barua CAG akimtaka afike mbele ya kamati hiyo ya Bunge kuhojiwa kutoka na kauli yake aliyoitoa akiwa anahojiwa na Idhaa ya Kiswahili ya Umoja wa Mataifa,  kuwa Bunge la Tanzania ni dhaifu.


from MPEKUZI

Comments