Bodi ya ushauri ya Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA) imetembelea eneo la Mradi wa ujenzi wa Maghala na Vihenge vya kisasa Mkoani Manyara na kuipongeza kampuni ya Unia Araj Realizacje Sp.o.o) chini ya msimamizi wa utekelezaji wa mradi huo ambaye ni Wakala wa Majengo Tanzania (TBA) kwa kasi waliyoanza nayo ya ujenzi.
Kampuni hiyo ambayo imeanza ujenzi huo tarehe 15 Disemba 2018 katika Halmashauri ya Mji wa Babati Mkoani Manyara katika kipindi hicho imetekeleza mradi huo kwa kasi nzuri, Imesema Bodi hiyo.
Mradi huo katika Kanda ya Arusha (Babati), pamoja na Dodoma, Makambako, Mbozi, Shinyanga, Songea, Sumbawanga na Mpanda. utagharimu Dola za Kimarekani Milioni 55, ikiwa ni mkopo wa masharti nafuu kutoka Serikali ya Poland ikiwa ni sehemu ya kiasi cha milioni 110 kilichotolewa kwa serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Akizungumza na mkandari wa mradi huo Mwenyekiti wa Bodi ya ushauri ya Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA) Mhandisi Eustance Kangole alisema kuwa kampuni hiyo inapaswa kuongeza kasi zaidi ya ujenzi ili kukamilisha kwa muda uliopangwa.
Alisema kuwa Hifadhi ya Chakula inayohitajika kukidhi mahitaji ya dharula kwa miezi mitatu ni zaidi ya tani 500,000 ukilinganisha na tani 150,000 iliyokuwa inahitajika miaka ya 1992 Wakala ulipoanzishwa.
Pia, technologia ya vihenge itawezesha Wakala kutumia teknolojia ya kisasa na hivyo kupunguza gharama za uendeshaji, Itawezesha Wakala kuhifadhi chakula kwa muda mrefu Zaidi, itasaidia kupunguza upotevu wa zao la mahindi baada ya kuvuna (posthaverst loss) na kuongeza soko la mahindi nchini na kuimarisha usalama wa nafaka inayohifadhiwa kwa kudhibiti sumukuvu (Aflatoxin) kwa mahindi yaliyohifadhiwa.
Bodi ya ushauri ya Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA) ikiongozwa na Mwenyekiti wa Bodi hiyo Mhandisi Eustance Kangole na katibu wake ambaye pia ni Kaimu Afisa Mtendaji mkuu wa Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA) Bi Vumilia L. Zikankuba imefanya ziara hiyo mara baada ya kikao kazi cha 33 cha Bodi hiyo Jijini Dodoma kilichofanyika kwa lengo la kujadili masuala muhimu ya Wakala ikiwemo utekelezaji wa mkataba wa mauzo ya mahindi Tani 36,000 kwa Shirika la Chakula Duniani (WFP) sambamba na kujadili maendeleo ya Mradi wa Vihenge na Maghala ya kisasa.
Vihenge 8 vinatarajiwa kujenzgwa Kanda ya Arusha katika eneo la (Babati) vyenye uwezo wa kuhifadhi nafaka Tani 25,000 ambapo pia yatajengwa maghala 2 yenye uwezo wa kuhifadhi nafaka Tani 15,000 hivyo kuwa na jumla ya Tani 40,000.
Baada ya mradi kukamilika Wakala utakuwa umeongeza uwezo wa kuhifahi kwa Tani 250,000 zaidi (vihenge vya kisasa 190,000 MT na maghala 60,000 MT) jambo ambalo litakuwa chachu na mafanikio yenye tija katika kuunga mkono Juhudi za utendaji wa serikali ya awamu ya tano inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt John Pombe Magufuli.
Kupatikana kwa Mradi huo nchini ni jitihada za Serikali ambazo zitapelekea ukuaji wa uchumi nchini na kuchangia kuwezesha Tanzania ya viwanda ambapo kutawezesha maghala ya Wakala kuweza kuhifadhi akiba ya Chakula ambayo itaendana na mahitaji halisi ya dharura kulinganisha na ongezeko la watu nchini.
MWISHO
from MPEKUZI
Comments
Post a Comment