Benki Ya NMB, Wizara Ya Mifugo Na Uvuvi Zaja Na Mikakati Zaidi Ya Uwekezaji Katika Sekta Ya Maziwa Nchini

Na. Edward Kondela
Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi anayeshughulikia Mifugo Prof. Elisante Ole Gabriel ameitaka Benki ya NMB kushirikiana na wizara hiyo katika kukuza sekta ya maziwa nchini kwa kuwa bado kuna mwitikio mdogo wa wananchi kunywa maziwa kutokana na taarifa iliyotolewa na Shirika la Chakula Duniani (WFP)

Prof. Gabriel amebainisha hayo leo (31.01.2019) Jijini Dodoma, akiwa kwenye kikao na maafisa kutoka idara ya kilimo ya Benki ya NMB, waliofika ofisini kwake kumwelezea mikakati ya Benki ya NMB ambayo imekuwa ikifanya tafiti na wadau wa sekta ya maziwa lengo likiwa ni kutaka kuwekeza katika sekta hiyo.

“Kwa takwimu ambazo zimetolewa na Shirika la Chakula Duniani ni kwamba kwa wastani angalau mtu anatakiwa walau atumie lita mia mbili kwa mwaka za maziwa lakini kwa bahati mbaya kwa watanzania wastani ni lita arobaini na saba tu, bado tuna kazi kubwa sana.” Alisema Prof Gabriel

Prof. Gabriel amesema Benki ya NMB inapaswa kuwa na ushirikiano na Wizara ya Mifugo na Uvuvi kupitia Dawati la Sekta Binafsi ambalo limekuwa likiwaunganisha wadau wa sekta ya mifugo na uvuvi, ili kuhakikisha mazao yatokanayo na ng’ombe yakiwemo maziwa yanatumika ipasavyo.

Katika kikao hicho ambacho kimehudhuriwa pia na watendaji wakuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Katibu mkuu huyo pia amesema ni wakati muafaka kwa Benki ya NMB kushirikiana na Wizara ya Mifugo na Uvuvi katika kuhakikisha inawaletea maendeleo wafugaji, hususan wafugaji wadogo ambao wamefanikiwa pamoja na wafugaji ambao watakuwa tayari kubadilika na kuingia katika ufugaji wa kisasa na kuachana na ufugaji wa kuhamahama.

Aidha Prof. Gabriel amesisitiza umuhimu wa kufanyika kwa tafiti kwa Wizara ya Mifugo na Uvuvi kwa kushirikiana na Benki ya NMB kupitia idara ya kilimo ili tafiti hizo ziweze kufanyiwa kazi na kuleta matokeo chanya kwa wafugaji.

“Ningependa sekta hii ya mifugo, iwe pia na tafiti nyingi zinafanyika, sasa tukifanya hizo tafiti tutaweza kuleta mabadiliko chanya na yenye uhakika katika maendeleo ya wafugaji kwa sababu lengo siyo tu kufanya jambo, lakini liwe jambo ambalo linaweza kugusa maisha ya wafugaji.”  Alisema Prof. Gabriel

Katika kikao hicho pia Katibu Mkuu Prof. Gabriel ameshauri uwepo wa mahusiano ya karibu kati ya Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Benki ya NMB na taasisi za elimu ya juu, ili kuhakikisha tafiti ambazo zimekuwa zikifanywa na wanafunzi ziweze kutumika katika kuleta mabadiliko na kuleta manufaa kwa wafugaji, badala ya tafiti hizo kuwekwa katika maktaba za vyuo hivyo pekee.

Kwa upande wake Meneja Mwandamizi wa Benki ya NMB kutoka idara ya kilimo Bw. Carol Nyagaro amesema kutokana na kasi ya utendaji kazi wa serikali ya awamu ya tano inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Magufuli pamoja na utendaji wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi imewalazimu benki hiyo kubadili mtazamo wa namna ya kutafuta wateja wapya kupitia sekta mbalimbali.

“Kutokana na kasi ya Mheshimiwa Rais Dkt. John Magufuli na uongozi mzima wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi, kwetu inajenga mazingira mazuri ya kufanya biashara, pia kuchangia maendeleo ya jamii na kuweza kutengeneza wateja wa siku zijazo.” Alisema Bw. Ngayaro

Aidha Bw. Nyagaro amesema Benki ya NMB kupitia idara ya kilimo inafikiria pia kuwekeza katika sekta ya samaki ambayo imekuwa ikifanya vizuri kiuchumi katika siku za hivi karibuni.

Bw. Nyagaro amemueleza pia Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi anayeshughulikia Mifugo Prof. Elisante Ole Gabriel, kuwa Muunganiko wa Vyama vya Ushirika Vikuu vya Maziwa Duniani unatarajia kufanya mkutano wake hapa nchini Tarehe 25 na 26 Mwezi Februari mwaka 2019 kwa kushirikiana na Benki ya NMB lengo kuu likiwa ni kuangalia uwezekano wa kuwekeza katika sekta ya maziwa hapa nchini.

Amefafanua kuwa muunganiko huo wenye nchi wanachama 95 ambao unafanya biashara ya takriban Dola za Marekani Bilioni 200 kwa mwaka, umeichagua Tanzania kwa ajili ya kufanya majadiliano kwa kuhusisha wadau wa sekta ya mifugo ili kuwekeza katika sekta ya maziwa.

Amesema mkutano huo pia utaainisha mambo ambayo tayari yalishafanyiwa tafiti kwa ajili ya utekelezaji wa mipango hiyo.

MWISHO.


from MPEKUZI

Comments