Serikali Kuwachukulia Hatua Kali Wamiliki wa Maabara Binafsi Wasiofuata Taratibu


Wamiliki wa maabara na vituo vya afya nchini wametakiwa kutimiza wajibu wao mara moja bila shurti kabla ya Januari 15 2019 kwa kuhakikisha wanakamilisha vigezo vyote vya umiliki maabara hizo kwa kuwa muda wa kutoa elimu umepita na sasa ni muda wa kazi tu.

Akizungumza na wanahabari leo jijini Dar es Salaam Mkurugenzi wa  Tiba wa Wizara ya afya, maendeleo ya jamii, jinsia, wazee na watoto na Mkurugenzi wa bodi ya usajili wa maabara Dkt. Dorothy Gwajima amesema kuwa hadi kufikia Septemba 2018 bodi ya usimamizi wa maabara binafsi ilitambua jumla ya maabara 641 zinazojitegemea na maabara 719 zilizoshikizwa kwenye vituo vya tiba vya watu binafsi vya ngazi mbalimbali.

Amesema kuwa kutokana na baadhi ya wamiliki wa maabara binafsi hasa zilizoshikizwa kutofuata maadili ya uwajibikaji kisheria kufikia Septemba 20, bodi kupitia ziara yake imebaini kuwa kati ya vituo vya tiba 1731vya  watu binafsi vyenye maabara ndani ni maabara 1012 sawa na asilimia 58 pekee ndizo zilizotimiza wajibu wake wa kujiandikisha kwenye bodi ya usimamizi wa maabara binafsi na kutekeleza matakwa ya kisheria.

Amesema kuwa wamiliki ambao hawatatekeleza wajibu wao wa kumiliki maabara hizo watachukuliwa hatua kali za kisheria ikiwemo kifungo pamoja na faini au vyote kwa pamoja.

Amewataka wamiliki hao kuhakikisha kuwa kila mmoja awe amekidhi vigezo vyote vya umiliki wa maabara ikiwa ni pamoja na kulipa ada zote stahiki zikiwemo malimbukizo ya nyuma na faini stahiki pamoja na kuwa na risiti halali za malipo hayo. Pia amewataka wamiliki wa maabara hizo kulipa tozo stahiki kila mwaka ili kuwezesha bodi kufanya uhakiki wa kudumu wa huduma zitolewazo katika maabara hizo.

Vilevile amesema kuwa katika kutekeleza hilo watatoa orodha za zahanati katika gazeti la Serikali na zahanati isiyokuwapo kwenye orodha hiyo haitatakiwa kutoa huduma yoyote na watakaokiuka watakutana na mkono wa dola. Gwajima ametoa mwito kwa serikali katika ngazi zote  kushirikiana na kutoa taarifa  dhidi ya wavunja sheria na kufanikisha  kuipeleka mbele sekta hiyo.

Akieleza kuhusiana na faini zitakazotolewa Kaimu Afisa msajili wa bodi ya usimamizi ya maabara binafsi Neema Halliye amesema kuwa kwa mujibu wa sheria watakaokiuka sheria hiyo watapigwa faini ya kulipa kiasi cha shilingi laki mbili au kufungwa miaka miwili au vyote kwa pamoja na bado maboresho ya sheria hiyo yanafanyiwa kazi ili kuweza kutoa kibano zaidi.


from MPEKUZI

Comments