Mama Mjamzito na Mwanae Wafariki Dunia kwa Uzembe wa Muuguzi...Mkuu wa Wilaya Atoa Siku Tatu

Mkuu wa Wilaya ya Igunga, John Mwaipopo
**
 Mkuu wa Wilaya ya Igunga, John Mwaipopo, ametoa saa 72 sawa na siku tatu kwa uongozi wa hospitali ya wilaya, kuwachukulia hatua kali watumishi wanaodaiwa kusababisha
kifo cha mjamzito.
 
Milo Peter (29), mkazi wa mtaa wa Masanga, Igunga, alifariki Desemba 29, mwaka huu na kuzikwa katika makaburi ya Masanga.
 
Baadhi ya wajawazito waliolazwa katika hospitali hiyo, waliwalalamikia watumishi wawili kufanya kazi kizembe, hali inayodaiwa kusababisha kifo cha Milo na mtoto.
 
Mbele ya diwani wa kata ya Igunga Charles Bomani, wajawazito hao, walidai mwenzao hakupata matibabu yanayostahili mapema, licha ya kuomba msaada kwa wauguzi waliokuwa zamu.
 
Kwa nyakati tofauti Blandina Enock, Rahel John, Rusia Ramadhani na Sikudhani Mrisho, walidai mwenzao alifikishwa hospitalini hapo Desemba 27, mwaka huu saa mbili usiku kwa ajili ya kujifungua.
 
Walisema kuwa, Milo alipofika alipewa kitanda huku ndugu zake waliomfikisha hospitalini, wakipewa ruhusa kuondoka.
 
"Jamani mnajua ufike wakati tuseme ukweli kwani kifo cha mama mwenzetu, kinaonekana kabisa uzembe umechangia.

"Sisi wenyewe tumeshuhudia kabisa namna ambavyo alikuwa akiomba msaada kwa wauguzi," alidai Rahel kwa niaba ya wenzake.
 
Kaimu Mganga Mkuu wa Wilaya ya Igunga, Amada Kasigwa, alikiri kutokea kwa kifo hicho cha mjamzito na mtoto mchanga mwenye uzito wa kilogramu 3.8.
 
Alisema kuwa vifo hivyo vilitokea Desemba 28, mwaka huu na kudai hali hiyo imetokana na uzembe wa muuguzi wa zamu, Matinde Muhonye. 

Kwa mujibu wa Amada, mtumishi huyo alionywa kuhusu madai hayo ya ufanyaji kazi kizembe.


from MPEKUZI

Comments