Katibu Mkuu CHADEMA Na Viongozi Wengine Wakamatwa Kwa Kufanya Mkusanyiko Bila Kibali

Jeshi la Polisi wilayani Hai, mkoani Kilimanjaro, linawashikilia Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Vincent Mashinji na viongozi wengine watatu wa chama hicho mkoani humo kwa tuhuma za kufanya mkusanyiko usio halali.

Mwenyekiti wa kamati ya ulinzi na usalama wilaya ya Hai ambaye ni mkuu wa wilaya hiyo, Lengai Ole Sabaya amesema viongozi hao wamekamatwa mchana.

"Ni kweli tumemkamata Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Mashinji, katibu wa Chadema mkoa wa Kilimanjaro, Basil Lema, mwenyekiti wa halmashauri ya Hai, Helga Mchomvu na msaidizi wa mbunge wa Hai, Freeman Mbowe, Irine Lema kwa kufanya mkusanyiko usio halali," amesema.

Sabaya amesema viongozi hao, leo mchana wamekutwa wakifanya mkusanyiko katika eneo la Boma bila ya kuwa na kibali jambo ambalo ni kinyume cha sheria.

"Naomba nitoe wito kwa wanasiasa kuheshimu sheria na taratibu, kama mnataka mkutano kuna taratibu hamuwezi kuvamia na kufanya mikutano kiholela," amesema.

Sabaya amesema katika wilaya yake ya Hai kwa sasa hataruhusu mikutano isiyo halali ambayo inalenga kuwapotosha wananchi kuhusu kazi nzuri ambazo zinafanywa na Rais john Magufuli.

"Waiache serikali ifanye kazi zake, kama wanataka siasa zao wasubiri kwenye kampeni, Hai tunataka maendeleo," amesema.



from MPEKUZI

Comments